Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahimiza ushirikiano zaidi wa maendeleo kimataifa wakati misaada ikipungua

Ban ahimiza ushirikiano zaidi wa maendeleo kimataifa wakati misaada ikipungua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amehimiza kuwepo ushirikiano zaidi wa kimataifa ili kupiga hatua katika kuyafikia malengo ya maendeleo ifikapo mwaka 2015, huku ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa ikionyesha kuwa kasi ya ufanisi ulofikiwa hadi sasa imo hatarini kupungua kwa sababu ya upungufu wa misaada.

Wakati akiizindua ripoti ya tume ya malengo ya milenia mwaka 2012, Bwana Ban amesema kuwa ripoti hiyo inatoa picha ya kusikitisha, na kwamba ni dhahiri kuwa kunahitajika ushirikiano kimataifa ili kuyafikia malengo ya milenia ifikapo mwaka 2015.

Malengo manane ya milenia yaliyokubaliwa na viongozi wa kimataifa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mwaka 2000, yalihusu hasa masuala ya kupunguza umaskini wa kupindukia, elimu, usawa wa kijinsia, afya ya uzazi na watoto, kuimarisha mazingira, kupunguza HIV na UKIMWI, na ushirikiano wa kimataifa wa maendeleo. Bwana Ban amerejelea ujumbe wake kwa jamii ya kimataifa kuwa, isiwafanye watu maskini zaidi kuubeba mzigo wa mdororo wa uchumi.