Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahiga alaani vikali shambulizi kwenye hoteli Somalia

Mahiga alaani vikali shambulizi kwenye hoteli Somalia

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia, Augustine Mahiga, amelaani vikali shambulizi lililoilenga hoteli ya Jazeera mjini Mogadishu, ambako rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alikuwa akifanya mkutano na waandishi wa habari. Tukio hilo limetokea wakati rais Hassan Sheikh akikutana na waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Samuel Ongeri, wakiwepo waandishi wa habari wa kimataifa.

Ripoti za awali zilisema kuwa washambulizi watatu wa kujitoa mhanga, na ambao walivalia sera za jeshi la Somalia, walijaribu kuingia kwenye hoteli hiyo, karibu kilomita nne kutoka mji mkuu Mogadishu, na kwamba walikabiliwa na vikosi vya usalama na kuuawa kabla ya kuingia hotelini. Baadhi ya walinzi wa usalama wa Somalia walijeruhiwa katika shambulizi hilo, na inasemekana mwanajeshi mmoja wa vikosi vya Muungano wa Afrika, AMISOM aliuawa, na watatu wengine kujeruhiwa.

Balozi Mahiga amesema kuwa shambulizi hilo limetokea siku mbili tu baada ya kuchaguliwa kwa rais Hassan Sheikh na bunge la Somalia, na kulipa taifa hilo matumaini mapya ya ufanisi katika siku zijazo. Ametuma rambi rambi zake kwa jamaa wa waliouawa katika shambulizi hilo, na kutoa heko kwa wanajeshi wa AMISOM kwa kujitolea kwao kulinda harakati za kisiasa.