Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahimiza serikali zisaidie jamii zilizobaki nyuma kujua kusoma na kuandika

Ban ahimiza serikali zisaidie jamii zilizobaki nyuma kujua kusoma na kuandika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ametoa wito kwa nchi kote duniani kufanya juhudi za haraka ili kuwafikia watu katika jamii zilizobaki nyuma na kuwasaidia wajue kusoma na kuandika. Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kujua Kusoma na Kuandika Septemba 8, Bwana Ban amesema kuwa hatua kubwa zimepigwa katika kipindi cha mwongo wa kujua kusoma na kuandika wa Umoja wa Mataifa, ambao unahitimishwa mwaka huu.

Katika kipindi hicho, Bwana Ban amesema takriban vijana milioni 90 wamejua kusoma na kuandika, na kwamba takwimu zikiendelea kwa mwenendo huo, zinatoa msukumo katika juhudi za kufikia mojawepo ya malengo ya maendeleo ya milenia, na kujenga jamii yenye ufahamu inayohitajika kwa karne ya 21.

Mwongo wa kujua kusoma na kuandika wa Umoja wa Mataifa ulizinduliwa mwaka 2003, na unatoa msingi na chagizo la kuongeza viwango vya kujua kusoma na kuandika kote duniani. Hata hivyo, takriban vijana milioni 775 bado hawawezi kusoma au kuandika, na watoto milioni 122 wenye umri wa kwenda shule hawaendi shule.