Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa UM kwenye michezo ya Olympics “Michezo ya mwaka huu ilivuka viwango”

Ujumbe wa UM kwenye michezo ya Olympics “Michezo ya mwaka huu ilivuka viwango”

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwa London kwenye michuano ya Olimpiki umesifu mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye michezo ya mwaka huu hatua ambayo wameeleza kuwa inafungua njia ya kupatikana mafanikio zaidi kwenye maeneo yanayohusu ustawi wa kijamii ikiwemo ujenzi wa amani na kupunguza matabaka ya kijinsia.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ujumbe huo umewapongeza waandaaji wa michezo hiyo, wanamichezo wenyewe, watazamaji na makundi ya watu yaliyojitoa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali katika kipindi chote cha michezo hiyo.

Umesema katika kipindi chote cha siku 17 kumeshuhudiwa mambo mengi ya kutia moyo yakifanyika jambo ambalo limeacha alama mpya ya kihistoria kuhusiana na michezo hiyo.

Jambo jingine lilipigiwa mfano na ujumbe huo ni kujitokeza kwa wanariadha wa kike kutoka katika nchi ambazo hapo awali zilipiga marafuku kwa wanawake kujitokeza kwenye michezo hiyo. Kwa mara ya kwanza mwaka huu mataifa kadhaa ikiwemo Saudi Arabia yaliruhusu wanamichezo wake wa kike kushiriki.