Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNSMIS ahimiza pande zote Syria kuwazia mazungumzo badala ya migogoro

Mkuu wa UNSMIS ahimiza pande zote Syria kuwazia mazungumzo badala ya migogoro

Mkuu mpya wa Waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria UNSMIS, ametoa wito yazingatiwe mawazo ya mazungumzo badala ya mawazo ya malumbano na nguvu za kijeshi.

Luteni Jenerali Babacar Gaye amesema hayo wakati akikutana na waandishi wa habari katika mji mkuu, Damascus, siku ya Jumatatu, baada ya ziara yake Homs na ar-Rastan siku ya Jumapili.

Amesema kuwa mjini Homs, amejioenea mwenyewe mashambulizi ya makombora mazito na mizinga kwenye vitongoji vya mji huo. Ameelezea pia kusikitishwa kwake na machafuko yanayoendelezwa sasa na pande zote husika katika mji wa Aleppo.

 "Natoa wito kwa pande zote, kama alivyosema mwakilishi maalum wa pamoja, kutulia na kuzuia umawagaji damu zaidi. Ni muhimu pande zote ziheshimu sheria ya kimataifa na kuwalinda raia. Naona ni muhimu kuacha haya mawazo ya malumbano na nguvu za kijeshi na kuwa na mawazo ya mazungumzo, kwanza katika ngazi ya vijijini, kisha kwenye ngazi ya kitaifa, ambayo yamechagizwa na mpango wa vipengee sita."

Mpango wa amani wenye vipengee sita uliwekwa na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu, Kofi Annan, kama njia ya kutafuta suluhu ya amani na kuwela serikali ya mpito, ambayo ingeongoza kurejeshwa kwa mfumo wa kidemokrasia na kikatiba, na unaoridhisha matakwa ya watu wa Syria.