Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa Watu Kufanya Mikutano Umebanwa sana nchini Kazakhstan:Pillay

Uhuru wa Watu Kufanya Mikutano Umebanwa sana nchini Kazakhstan:Pillay

Uhuru wa watu kukutana na kufanya maandamano umebanwa sana nchini Kazakhstan na sheria za mwaka 1995 zinapaswa kubadilishwa ili ziende sambamba na viwango vya kimataifa, amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay. Kwa mujibu wa Bi Pillay, wanaoandaa maandamano na mikutano ya hadhara nchini humo huwajibika kwa usalama wa mikutano kama hiyo, na kutozwa faini kali machafuko yakitokea.

Bi Pillay anasema, kuhakikisha usalama ungelikuwa wajibu wa polisi na sio waandamanaji. Amesema sheria kama hiyo inaweka wazi nafasi ya ukiukaji wa sheria, kwani huwapa motisha wapinzani wa waandamanaji kuchochea ghasia ili kuwafanya waandamanaji wasiweze kufanya hivyo.

Amesema pia makundi yanayotaka kufanya maandamano hutakiwa kutimiza masharti fulani ya utaratibu, ambayo ni magumu kutimiza, hali ambayo inabana uwezo wa watu kufurahia uhuru huo muhimu wa kukutana au kufanya maandamano.