Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa ulokuwa Ukiwaua Watoto Cambodia Watambuliwa:WHO

Ugonjwa ulokuwa Ukiwaua Watoto Cambodia Watambuliwa:WHO

Kilichowaua zaidi ya watoto 50 nchini Cambodia, sasa kimetambuliwa kuwa aina hatari ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa mikono, miguu na midomo, ambao hupatikana hasa miongoni mwa watoto. Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema aghalabu ugonjwa huo huwa ni wenye athari ndogo na wenye dalili zisizo ngumu kutambuliwa.

Lakini, kutegemea ni aina gani ya virusi vinavyohusika, ugonjwa huu huwa hatari sana na hata kusababisha kifo. Ugonjwa huo huwaathiri watoto chini ya miaka 10, na dalili zake huwa ni homa, vidonda vinavyouma sana mdomoni, na malengelenge kwenye mikono, miguu na makalio. WHO inasema kuwa inashirikiana na serikali ya Cambodia ili kuendeleza ufahamu wa usafi miongoni mwa umma, na hasa faida za kunawa mikono mara kwa mara. WHO inasema ugonjwa huo ni tofauti kabisa na ugonjwa wa shuna unaoathiri mifugo.