Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iran yafaa Kuhusishwa Katika Kutafuta Suluhu kwa Mzozo wa Syria:Annan

Iran yafaa Kuhusishwa Katika Kutafuta Suluhu kwa Mzozo wa Syria:Annan

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Kiarabu kuhusu mzozo wa Syria, Kofi Annan, amesema Iran inatakiwa kuhusishwa katika kutafuta suluhu kwa mzozo wa Syria. Bwana Annan ambaye amekuwa Tehran kufanya mazungumzo na viongozi wa Iran kuhusu mzozo wa Syria, amesema mchakato mzima wa kisiasa ambao unatakiwa kuwaleta wahusika wote pamoja bado haujaanza.

Annan amesema kwenda kwake Iran kunaashiria kile ambacho amekuwa akizungumzia mara kwa mara, na imani yake kwamba Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika harakati za kutafuta suluhu kwa mzozo wa Syria. Ameongeza kuwa kuwaleta wahusika wote kwenye meza moja ya mazungumzo ni sehemu ya vipengee sita vya mpango wake wa amani.

Bwana Annan sasa yupo Baghdad kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki kuhusu mzozo wa Syria na athari zake kwa kanda nzima.