Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi ya Ndimbati yahamishiwa Rwanda

Kesi ya Ndimbati yahamishiwa Rwanda

Mahakama ya kimataifa kuhusu mauaji Rwanda, (ICTR), imeihamishia kesi dhidi ya mshukiwa Aloys Ndimbati nchini Rwanda ili isikilizwe huko. Aloys Ndimbati alikuwa mkuu wa jimbo la Gisovu tokea mwaka 1990 hadi mwishoni mwa Julai 1994 yalipomalizika mauaji ya kimbari. Ndibati, ambaye bado yupo mafichoni, ameshtakiwa kwa mauaji ya kimbari, kusaidia kutekeleza mauaji hayo, kuchochea mauaji hayo, pamoja na ubakaji na ukatili mwingine, ambayo yote ni uhalifu dhidi ya binadamu.

Hii ndiyo kesi ya saba kuhamishiwa Rwanda na mahakama hiyo ya ICTR. Katika uamuzi wa kuihamishia kesi ya Ndimbati Rwanda, majaji wakuu ICTR, wakiongozwa na Vagn Joensen, waliamuru kuwa kesi hiyo iwekwe chini ya mamlaka ya serikali ya Rwanda, ambayo itaipeleka kwenye mahakama yake kuu.

Kiongozi wa mashtaka ameamrishwa kuwasilishia serikali ya Rwanda ushahidi wote uliopo dhidi ya Ndimbati katika kipindi cha siku 30. Katika kufanya uamuzi huu, mahakama ya ICTR inatumaini kwamba kwa kukubali kuziendesha kesi zinazohamishiwa kwake na mahakama hiyo, serikali ya Rwanda itatekeleza ahadi zake kuhusu uwezo na kujitolea kwake kuweka viwango vya juu vya kimataifa vya haki na sheria.