Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa UM akaribisha maafikiano kuhusu katiba Somalia

Mwakilishi wa UM akaribisha maafikiano kuhusu katiba Somalia

 

Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Makataifa kuhusu masuala ya Kisiasa nchini Somalia, ameukaribisha muafaka uliosainiwa na viongozi wa Somalia kama hatua muhimu katika kulitayarisha taifa hilo kwa ajili ya kumalizika mfumo uliopo sasa wa serikali ya mpito. Katika mkutano uliofanyika mjini Nairobi, Kenya, viongozi wa Kisomali wameafikia mswada rasmi wa katiba , ambao sasa utachapishwa.

Katika taarifa yake, Mwakilishi huyo maalum, Augustine Mahiga ameelezea kufurahishwa kwake na wahusika kuja pamoja kwa moyo wa ushirikiano na maridhiano, na kukubali kwa kauli moja kuendeleza harakati hizi za kisiasa. Amesema na hakuna muda wa kupoteza.

Baada ya miongo ya vita, nchi ya Somalia imekuwa kwenye harakati za amani na maridhiano, huku taasisi zake za mpito zikitekeleza mpango wa kuhitimisha kipindi cha mpito, ambao ulikubaliwa mwezi Septemba mwaka uliopita, na ambao unaweka masuala muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele kabla ya kumalizika kwa mfumo wa serikali ya mpito Agosti 20.