UM Washerehekea Kupiga Hatua Katika Kampeni ya Kukiuka Haki za Watoto
Umoja wa Mataifa umesherehekea kupiga hatua katika kampeni ya kutia saini mikataba ya ziada kuhusu haki za watoto. Tangu kampeni hiyo ya uwekaji saini kote duniani ilipozinduliwa miaka miwili iliyopita, mataifa 20 zaidi yametia saini mkataba wa zaida kuhusu uuzaji wa watoto, kuwahusisha katika biashara ya ngono, na katika ponografia. Mataifa mengine 15 yamejiunga kwenye mkataba wa ziada unaohusu kuwahusisha watoto katika mizozo ya vita.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Marta Santos Pais amesema kuwa lengo la jumla la kukamilisha kusaini mikataba hiyo ili kukomesha vitendo vya kikatili dhidi ya watoto na kuwalinda watoto kutokana na dhuluma, linakaribia kufikiwa.
Bado kuna mataifa 46 kote duniani ambayo hayajatia saini mkataba kuhusu kuwatumia watoto kama wanajeshi. Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Watoto katika maeneo ya vita, Radhika Coomaraswamy, ameongeza kuwa kuweka saini mkataba, kukifuatiwa na utekelezaji wa kina, kunaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maisha ya watoto walionaswa katikati ya mizozo, na ambao wanakabiliwa na hatari ya kunyanyaswa. Ametoa wito kwa mataifa yaliyo kwenye mizozo yaweke saini mkataba kwa haraka, na yale yenye amani, yafuate mkondo huo, kama ishara ya kukomesha tabia inayoaibisha ya kuwaingiza watoto katika vita.