Kingamo za kisiasa bado ni kizuizi kwa kulinda Haki za Binadamu Zimbabwe:Pillay

25 Mei 2012

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema kuwa, ingawa kuna serikali ya muungano wa vyama vitatu vikuu nchini Zimbabwe, bado kuna kingamo au uadaui wa bayana baina wa kisiasa nchini humo. Akiwahutubia waandishi wa habari wakati akikamilisha ziara yake ya kwanza nchini humo, Bi Pillay amesema kuwa kingamo hizi zilizopo hivi sasa ni kizuizi kikubwa kwa maswala muhimu, ikiwemo kulinda na kuimarisha haki za binadamu.

Bi Pillay ameongeza kuwa kuna hofu ndani na nje ya Zimbabwe kuwa, endapo vyama husika havitakubaliana kufanya mageuzi Fulani muhimu na watu kubadili mitazamo yao, basi uchaguzi ujao hapo mwakani huenda ukawa kama ule wa mwaka 2008- ambao ulisababisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ukiwemo mauaji, utesaji, ubakaji, kuwazuilia watu kinyume na sheria, pamoja na kuwalazimu wengine kukimbia makwao.

Bi Pillay pia ametoa wito kwa serikali ya mpito ya Guinea Bissau kuheshimu haki za binadamu. Amesema, ingawa viongozi wa kijeshi waliukabidhi uongozi kwa serikali ya mpito ya umma kufuatia kusaini mkataba wa makubaliano, bado anasikitishwa na ripoti za ukiukaji wa haki za binadamu, zikiwemo ukandamizaji, unyang’anyi na kuwazuilia raia kinyume na sheria. Ameongeza kuwa yeyote aliyefanya ukiukaji huu ni sharti achukuliwe hatua za kisheria.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter