Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa UM Sudan akaribisha kuendelea kuwasafirisha raia wa Sudan Kusini

Mratibu wa UM Sudan akaribisha kuendelea kuwasafirisha raia wa Sudan Kusini

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan Bwana Ali Al-Za’tari amekaribisha mchakato unaoendelea wa kuwahamisha kwa ndege kutoka Khartom kuelekea Juba raia takribani 12,000 wa Sudan kusini waliokuwa wamekwama kwa miezi kadhaa eneo la Kosti wakisubiri usafiri.

Safari hizi zinasimamiwa na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM na kusaidiwa na serikali ya Sudan Kusini. Mpango wa kuwasafirisha watu hao ulianza wiki moja iliyopita na hadi sasa wameshasafirishwa watu 4200 hadi Sudan Kusini.

Bwana Al-Za’tari amesema anakaribisha ushirikiano baina ya serikali za Sudan na Sudan Kusini katika kufanikisha zoezi hilo. Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa itaendelea kuelekeza juhudi zake katika kuwasaidia watu wa Sudan Kusini.