Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi ya Kakuma yashuhudia wimbi la wakimbizi kutoka Sudan na Sudan Kusini:UNHCR

Kambi ya Kakuma yashuhudia wimbi la wakimbizi kutoka Sudan na Sudan Kusini:UNHCR

 

Kambi ya wakimbizi ya Kakuma iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Kenya imeanza kushuhudia tena wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Sudan na Sudan Kusini.

Kambi hiyo ilianzishwa mwaka 1992 kwa ajili ya wakimbizi wa Sudan kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vikiendelea, lakini kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR miaka 20 baadaye kambi hiyo inapokea tena wakimbizi wanaokimbia vita katika baadhi ya sehemu za Sudan na Sudan Kusini.

Zaidi ya watu 4500 wamewasili katika kambi ya Kakuma  mwaka huu huku zaidi ya asilimi 76 wakitokea Sudan na Sudan Kusini, wengi wakidai kukimbia mapigano katika jimbo la Jonglei, wakizungumzia mashambulizi ya kulengwa, wizi wa ng’ombe na kuchomwa kwa nyumba zao.

Kwa mujibu wa UNHCR familia nyingi zimetenganishwa na machafuko, na baadhi ya vijiji vikisalia tupu bila watu Jonglei.

Wakimbizi wengine waliowasili karibuni wanatoka jimbo la Kordofan Kusini ambako mapigano yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa kati ya majeshi ya Sudan na wapiganaji wa SPLM-North.