Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna haja ya kuwa na mashirikiano kushinda hujma za kiharamia Pwani ya Guinea-UM

Kuna haja ya kuwa na mashirikiano kushinda hujma za kiharamia Pwani ya Guinea-UM

Kuna haja ya kuweka mikakati ya dharura kukabiliana na ongezeko la vitendo vya uharamia katika pwani ya Guinea, na hii itazaa matunda kama nchi husika zimedhamiria kuzishinda hujma za maharamia hao.

Akijadilia tishio la kiusalama pamoja na maendeleo ya kiuchumi kwenye eneo hilo, mwakilishi wa Katibu Mkuu katika masuala ya kisiasa Lynn Pascoe amesema kuwa nchi zilizopo kwenye ukanda huo zinapaswa kutambua kuwa mashirikiano ya pamoja ndiyo silaha maalumu itayoweza kuwashinda maharamia hao.

Amesema nchi hizo zinapaswa kuunganisha nguvu kukabiliana na ongezeko la vitendo vya uharamia, lakini kutegemea nguvu ya nchi moja pekee, hakuwezi kuleta suluhisho la kudumu.

 Mwanadiplomasia huyo alikuwa akitoa taarifa mbele ya wajumbe wa baraza la usalama kuhusiana na hali ya mambo katika eneo la pwani ya Guinea ambayo kwa sasa inaandamwa na ongezeko la vitendo vya uharamia.