Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani kuuawa kwa mwanajeshi wa Nigeria huko Darfur

Ban alaani kuuawa kwa mwanajeshi wa Nigeria huko Darfur

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani kuuawa kwa mwanajeshi mmoja wa Nigeria na kujeruhiwa kwa wengine watatu katika shambulio dhidi ya vikosi vya pamoja vya Umoja wa Maitaifa na Muungano wa Afrika vinavyolinda amani katika eneo la Darfur, nchini Sudan UNAMID.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Ban, washambuliaji wasiojulikana waliwavizia wanajeshi wa UNAMID waliokuwa katika doria karibu na eneo la Saleah, siku ya Jumamosi.

Ban ameitaka serikali ya Sudan kuchunguza kisa hicho haraka na kuhakikisha kuwa waliohusika na uhalifu huo wamekamatwa, pia ametoa rambarambi zake kwa serikali ya Nigeria na familia ya mwanajeshi aliyeuawa.

Mkuu wa UNAMID, Ibrahim Gambari, naye amelaani shambulio hilo na kusisitiza kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani ni uhalifu wa kivita. Walinda amani 35 wamepoteza maisha yao katika eneo la Darfur tangu UNAMID ilipoanza operesheni zake 2007.