Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani 600,000 wanakabiliwa na shida Haiti:Amos

Wakimbizi wa ndani 600,000 wanakabiliwa na shida Haiti:Amos

Takriban wakimbizi wa ndani 600,000 waliosambaratishwa na tetemeko la ardhi la mwaka jana nchini Haiti wako katika hatari ya kukabiliwa na njaa, kipindupindu na majanga ya asili amesema mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa.

Valarie Amos ambaye amerejea kutoka Haiti alikozuru kwa siku mbili amesema uongozi wa taifa hilo la Caribbean, watu wa nchi hiyo na wahisani wanataka kuona mtazamo na juhudi kubwa katika maendeleo.

Amesema ingawa idadi ya wakimbizi wa ndani imepungua kutoka milioni 1.5 mwaka jana, lakini mahitaji muhimu ya kibinadamu bado yapo na yanahitaji kushughulikiwa.

Amekutana na baadhi ya wakimbizi hao kwenye kambi ya Accra ambapo wamemueleza adha zinazowakabili kwa kuishi kambini hapo kwa muda mrefu, wanataka kuondoka lakini hawawezi kumudu kulipa kodi au kukarabati nyumba zao.

Watu 250,000 walikufa katika tetemeko hilo, ambalo pia lilisambaratisha kabisa miundo mbinu.