Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu la UM lapinga ghasia dhidi ya walio na maisha tofauti ya kingono

Baraza la haki za binadamu la UM lapinga ghasia dhidi ya walio na maisha tofauti ya kingono

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeelezea kusumbuliwa kwake kuhusu dhuluma na ubaguzi wanaopitia watu kutokana na maisha yao ya kingono na kutoa wito wa kufanywa uchunguzi wa kimataifa kuonyesha shida wanazopitia.

Kwenye azimio lililopitishwa mjini Geneva baraza hilo liliomba ofisi ya kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuendesha utafiti ifikapo mwezi Disemba mwaka huu kuonyesha sheria zinazobagua na vitendo vingine vya dhuluma dhidi ya waliojiamulia maisha yao ya kingono kote duniani. Nchi 23 ziliunga mkono kupitishwa kwa azimio hilo huku 19 zikilipinga.

Mwezi mmoja uliopita kamishina wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay alisema kuwa uovu unaotendwa dhidi ya mashoga , watu wenye jinsia mbili na wanaobadili jinsia unazidi kuongezeka duniani.