Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia lazima walindwe na athari za vita:Baraza la usalama

Raia lazima walindwe na athari za vita:Baraza la usalama

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo kwa mara nyingine limetoa wito kwa pande zinaziohusiaka katika vita kuchukua hatua za kuwalinda raia kutokana na athari za machafuko.

Limezitaka kukomesha vitendo cvya ubakaji, kushinikiza watu kuingia jeshini na ukiukaji mwingine wa haki na sheria za kimataifa za binadamu. Katika taarifa maalumu ya Rais wa baraza iliyotolewa wakati wa mjadala kuhusu suala hilo baraza limeelezea hofu ya athari za vita kwa raia na limezitaka pande zinazohusika na mapigano kuwalinda raia kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

Wajumbe 15 wa baraza hilo pia wamerejea kusema pande zinazohusika na machafuko zinawajibika kuchukua hatua muhimu za kuhakikisha zinawalinda raia. Katika ripoti yake ya karibuni kuhusu suala hilo kwenye baraza la usalama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesisitiza haja ya kuleta mabadiliko katika maisha ya maelfu ya raia wanawake, wanaume na watoto wanaokabiliwa na jinamizi la vita katika maisha yao ya kila kila siku.

Ban ameongeza kuwa makundi ya wanamgambo wenye silaha wanatumia mbinu zinazokiuka sheria za kimataifa ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya raia, ubakaji, kushambulia vituo vya raia kama shule, utekeji, kuwalazimisha na kuwatumia raia kama ngao wakati wa vita na kuwaingiza watoto jeshini.

Amesema pande zote lazima ziwajibike kuwalinda raia kwa kueshimu na kuzingatia sheria za haki za binadamu.