Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeleeza wasi wasi wake baada ya kutekwa nyara mtetea haki za binadamu Kongo

UM umeleeza wasi wasi wake baada ya kutekwa nyara mtetea haki za binadamu Kongo

Afisi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO imeeleza wasi wasi wake kutokana na kile kinachoaminika ni kutekwa nyara mtetea haki za binadam aliyezungumza dhidi ya ukiukaji wa haki za binadam unaofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo.

Sylvestre Bwira Kyahi, rais wa kundi la kiraia la haki za binadam huko Masisi alionekana mara ya mwisho mjini Goma mji mkuu wa jimbo lenye ghasia la Kivu ya Kaskazini hapo Agosti 24.

Taarifa ya MONUSCO iliyotolewa jana inaeleza kwamba watu wawili wanaripotiwa wakiwa na mavazi ya kijeshi walimlazimisha Bw Kyahi kupanda ndani ya gari la kijeshi.

Afisi hiyo inatoa wito kwa maafisa wa Kongo kufanya kila wawezalo kusitisha vitisho, bughudha na vitendo vingine vya kuwanyanyasa watetezi wa haki za binadam kote nchini DRC.

Bw Bwira Kyahi amekua akikabiliwa na vitisho na kunyanyaswa siku za nyuma hasa baada ya kuchapisha barua wazi mwezi uliyopita inayowatuhumu wanajeshi wa serikali huko Masisi kwa ukiukaji wa haki za binadam na kutaka wahamishwe.