Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo la UM la mabadiliko ya hali ya hewa lasema ripoti ya tathmini huru itasaidia kazi zake

Jopo la UM la mabadiliko ya hali ya hewa lasema ripoti ya tathmini huru itasaidia kazi zake

Katibu Mkuu Ban Ki-moon amepongeza kazi za baraza huru la wasomi IAC kutathmini matokeo ya jopo la ushirikiano wa serikali juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, IPCC.

IPCC ilikosolewa vikali 2007 baada ya kutoa tarehe isiyo sawa kwamba theluji kwenye mlima Himalaya huwenda ikayayuka kabisa ifikapo 2035. Kutokana na hayo Katibu Mkuu pamoja na mkuu wa IPCC Rajendra Pachauri waliteua baraza huru la wasomi wa sayansi kutathmini utafiti wao na hii leo katika mkutano mjini New York walimkabidhi Bw. Ban na ripoti yao kamili.

Bw. Ban amesema anatazamia kusoma mapendekezo ya tathmini iliyofanywa na kuhimiza serikali 194 wanachama wa IPCC kutafakari kwa makini matokeo ya IAC na kuchukua hatua zinazostahiki kwa haraka iwezekanavyo. Katibu  Mkuu alishikilia kwa dhati kwamba misingi ya sayansi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa ingali thabiti. Na anaendelea kuunga mkono matokeo ya ripoti ya nne ya IPCC ambayo imekubaliwa na wataalamu mbali mbali kote duniani.