Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwe na sheria kali dhidi ya mamluki na makampuni binafsi ya ulinzi:UM

Kuwe na sheria kali dhidi ya mamluki na makampuni binafsi ya ulinzi:UM

Kundi la wataalamu binafsi wa Umoja wa Mataifa dhidi ya matumizi ya askari maluki wanasema watawasilisha pendekezo la kuwepo mkataba wa kimataifa ili kufuatilia shughuli binafsi za kijeshi na makampuni ya ulinzi.

Katika mkutano wao wa siku tano kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York, kundi hilo litawapa taarifa za kina mabalozi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wanazuoni kuhusu mapendekezo yao yenye lengo la kuziba pengo la kisheria ambalo limekuwa likifumbia macho shughuli za maluki katika ngazi ya kimataifa. Tangu kuanzishwa kwa kundi hilo la wataalamu mwaka 2005 limekuwa kilifuatilia athari za shughuli za askari mamluki na makampuni binafsi ya ulinzi katika haki za binadamu na hususani kutowajibika kwao.

Pendekezo la kundi hilo linatoa wito wa sheria kali zitakazoangalia na kufuatilia masuala ya askari maluki na makampuni binafsi ya ulinzi katika ngazi ya taifa na kimataifa. Kundi hilo la wataalamu litatoa ripoti ya hatua walizopiga za uwezekano wa mswada utakaojadiliwa kwenye baraza la haki za binadamu Septemba 14 mwaka huu na pia kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa.