Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Tarehe ya 18 Disemba huadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa kwa Wahamaji. Risala ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), iliowasilishwa kuadhimisha siku hii, ilihimiza mataifa kuonyesha bidii za mbele zaidi, kupita Mkutano wa Copenhagen, na kukabili masuala magumu ya uhamaji unaochochewa na uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa hali ya hewa. Taarifa ya IOM ilieleza wanasayansi wa kimataifa walishathibitisha kihakika kwamba mabadiliko ya hali ya hewa na uchafuzi wa mazingira ni mambo yanayozusha uhamaji wa dharura na kusababisha watu kung\'olewa mastakimu, katika sehemu mbalimbali za dunia, hasa katika nchi masikini, maeneo ambayo ndio yenye kudhurika zaidi na maafa ya kimaumbile. Kwa mujibu wa IOM kuna pengo kubwa la maarifa na uzoefu juu ya ujuzi unaofaa kushughulikiwa, ili kudhibiti vyema matokeo na athari kubwa za uhamaji unaoletwa na maafa ya kimazingira.