KM ana matumaini juu ya itifaki ya kupunguza utoaji wa gesi chafu angani

8 Disemba 2009

KM Ban Ki-moon kwenye mahojiano na gazeti la kila siku la Denmark, linaloitwa Berlingske Tidende - yaliochapishwa Ijumapili, alisema ana "matarajio ya matokeo mazuri kutokana na majadiliano ya wawakilishi wa kimataifa" kwenye mkusanyiko wa Copenhagen.

Alisisitiza kwamba anaamini "mapatano yatapatikana na kutiwa sahihi na Mataifa Wanachama wote wa UM, kitendo ambacho kitawakilisha hatua ya kihistoria," alitilia mkazo. Wajumbe kutoka nchi 190 waliwasili Copenhagen mnamo mwisho wa wiki kuhudhuria Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, na wanatazamiwa kukamilisha mapatano mapya ya kimataifa, yatakayorithi Mkataba wa Kyoto, ambao muda wake utamalizika mwaka 2012. Rajendra Pachauri, Mwenyekiti wa Tume ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (IPCC), yeye kwa upande wake, alitilia mkazo kwenye hotuba aliowakilisha kwenye ufunguzi wa mkutano ya kuwa "ushahidi wa kisayansi juu ya taathira za mabadiliko ya hali ya hewa, umeshathibitishwa kupitia kiasi, na ulimwengu utafaidika pakubwa ukichukua hatua za mapema kukabiliana na tatizo hili, au si hivyo gharama za kiuchumi na kwa wanadamu, zitarundikana na kukithiri nje ya uwezo wa kimataifa kuzimudu, katika siku za baadaye." Hivi sasa wapatanishi wamebakiza siku sita kumaliza majadiliano yao kabla ya kufanyika Sehemu ya Pili ya kikao, kinachotarajiwa kuanzisha mashauriano katika tarehe 16 Disemba (2009). Jumla ya wajumbe 15,000 sasa hivi wanahudhuria Mkutano wa Copenhagen, wakiwakilisha serikali, mashirika ya kibiashara, viwanda na jumuiya zinazotetea hifadhi ya mazingira, na kutoka taasisi za utafiti zinazoshughulikia udhibiti wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud