Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ripoti ya KM aliotumia Baraza la Usalama siku ya leo, imeelezea hali mpakani kati ya Syria na Israel ya kuwa ni shwari, kwa ujumla. KM amependekeza kwenye ripoti zile operesheni za Vikosi vya UM vya Uangalizi wa Kusimamishwa Mapigano kwenye Milima ya Jolan Syria (UNDOF) ziongezewe muda wa shughuli zake kwa miezi sita ziada - hadi mwezi Juni 2010.

Risala ya KM Ban Ki-moon kuhishimu Siku ya UKIMWI Duniani, siku ilioangukia tarehe ya leo - 01 Disemba 2009 - ilieleza kuwa kunatakikana mchango ziada, wa dharura, kutumika kimataifa ili kuhakikisha ahadi ya kila mtu ulimwenguni kupatiwa uwezo wa kujikinga na VVU, pamoja na kupatiwa uuguzi na misaada ya kutunza mgonjwa wa maradhi hayo, itatimizwa, pakihitajika, itakapotimu 2010. Alisema miradi hii itaweza kufikiwa pindi haki za binadamu za watu wote wanaoishi na VVU zitahishimiwa kimataifa, pamoja na haki za umma unaohatarishwa na maambukizo ya virusi, ikijumlisha watoto na wazee wao walioathirika na janga la maradhi. Kadhalika KM alizisihi nchi zote za dunia kufuta sheria zenye kuadhibu wagonjwa wa UKIMWI, na kukomesha haraka sera zao na zile tabia zinazowazuia watu waliopatwa na VVU kuhudumiwa afya, ikijumlisha vikwazo vya kusafiri kwa matibabu au shughuli nyengine.

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM kwa Haki za Binadamu, leo amesema vikwazo vya taifa la Uswiss dhidi ya ujenzi wa minara ya misikiti nchini ni dhahiri kitendo cha kibaguzi chenye kuchochea na kuleta mgawanyo mkubwa miongoni mwa jamii. Kwenye taarifa aliotoa kuhusu uchaguzi wa Ijumapili, ambapo kura ya maoni ilipendekeza minara isijengwe kwenye misikiti ya Uswiss, Bi. Pillay alieleza ya kuwa anaamini uamuzi huo ulikuwa ni "hatua ya kusikitisha" kwa taifa la Uswiss, na unahatarisha kuzusha mgongano juu ya utekelezaji wa majukumu yaliodhaminiwa Uswiss na sheria za kimataifa juu ya haki za binadamu. Vile vile Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu alisema kura ya Uswiss, ambayo wakati wa kampeni iliendelezwa kwa kutumia mabango yenye kuonyesha chuki kali dhidi ya wageni, mwelekeo kama huo alisema unamtia wasiwasi mkubwa juu ya namna uhuru wa kidini unavyotekelezwa kwenye nchi. Alisisitiza siasa zinazotumia kigezo cha kupalilia chuki dhidi ya wageni, au utovu wa ustahamilivu kwa mila tofauti, popote zinapotekelezwa, ni vitendo vinavyofadhaisha na kutia wasiwasi mkubwa taasisi za UM zinazohusika na haki za binadamu. Kwa hivyo, Kamishna Mkuu Pillay aliusihi umma wa kimataifa kote ulimwenguni kuzingatia kidhati, hatua za dharura, ili uweze kukabiliana vyema na suala la ubaguzi wa wafuasi wa tamaduni tofauti.

Naibu KM wa UM, Asha-Rose Migiro, Ijumanne alihutubia mkutano juu ya Ushirikiano Miongoni mwa Mataifa ya Kizio cha Kusini ya Dunia uliofanyika kwenye mji mkuu wa Kenya wa Nairobi. Alipongeza ya kuwa ushirikiano wa mataifa haya ni uhusiano wenye kuhamasisha Mataifa Wanachama kuweka kando masilahi finyu ya kitaifa kwa faida ya wote. Alikumbusha ushirikiano huu umeanza kushuhudiwa katika shughuli za biashara, shughuli za kifedha na katika sekta ya teknolojiya, kadhia ambazo hujumlisha jumuiya mpya ya mataifa yenye uwezo wa kuwa na uchumi wenye nguvu. Alizihimiza nchi za Kusini kushirikiana zaidi vile vile kwenye shughuli za kutatua kipamoja yale masuala yanayohusu matatizo ya njaa, ukosefu wa ajira, mizozo ya uchumi wa dunia na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Alionya kwamba maendeleo hayatoweza kushuhudiwa kutoka hali ya pengo. Alizihimiza nchi husika kuwekeza zaidi na kubadilishana biashara miongoni mwa mataifa yao ya Kusini. Alikumbusha UM unaweza kutumiwa nao kuwa kama kichocheo cha kuimarisha ushikirikiano ulio bora miongoni mwa mataifa ya kizio cha Kusini ya dunia. Kadhalika, Helen Clark, Mkuu wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) alihutubia mkutano wa Nairobi, na aliwaambia wajumbe waliokusanyika huko ya kuwa lengo halisi katika kazi za taasisi ya UNDP ni kusaidia na kurahisisha uwezo wa nchi za Kusini kubadilishana maarifa na uzoefu ili ziweze kuhakarakisha zaidi ustawi wa maendeleo.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati, Ijumanne, alizuru nyumba ya WaFalastina, ilionyanganywa na kukaliwa kimabavu na walowezi wa Israel, katika eneo la Sheikh Jarrah, Jerusalem Mashariki. Baada ya ziara hiyo, ofisi ya Serry ilichapisha taarifa kwa vyombo vya habari yenye kueleza kwamba KM amechukizwa na kuendelezwa kwa vitendo vya kubomoa kihorera nyumba za WaFalastina, kuwang'oa kimabavu na kusiko halali kutoka mastakimu yao, na kitendo haramu cha kuwapa walowezi wa Kiisraili makazi hayo kwenye maeneo ya WaFalastina yaliopo Jerusalem Mashariki. Taarifa ya Serry ilisisitiza kwa mara nyengine tena kwamba KM anataka vitendo hivi haramu visitishwe haraka iwezekanavyo.