Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya raia wa Kihutu katika JKK yalaumiwa na Mtetezi wa Haki za Binadamu

Mauaji ya raia wa Kihutu katika JKK yalaumiwa na Mtetezi wa Haki za Binadamu

Philip Alston, Mkariri/Mtetezi Maalumu wa UM juu ya Haki za Binadamu dhidi ya Mauaji ya Kihorera Nje ya Sheria, hii leo ametoa taarifa maalumu kuhusu JKK.

Alisema kwenye taarifa yake kwamba ameweza kuthibitisha vikosi vya Serikali viliua makorija ya raia kwenye jimbo la mashariki la katika JKK, pale askari wake walipoendeleza operesheni za kuwan'goa makundi ya waasi wa kundi la FDLR, waasi ambao hujumuisha wauaji waliohusika na mauaji ya halaiki ya Rwanda, na ambao wamekutikana kushiriki kwenye vitendo vya kuchafua utulivu katika JKK. Karibuni Alston alifanya ziara ya siku kumi na moja katika sehemu mbalimbali za nchi, kuendeleza uchunguzi kuhusu matukio ya mauaji ya kihorera dhidi ya raia. Alisema kwenye taarifa yake askari wa JKK waliwadunga risasi, na kuwapiga mpaka kufa, wahamiaji 50 wa kutoka Rwanda, na kuchoma moto nyumba zao kwenye shambulio waliolifanya mwezi Aprili 2009. Kwenye tukio hilo, alisema vile vile wanawake 40 walitoroshwa kutoka kambi ya wahamiaji, 10 ya kundi hilo, waliofanikiwa kuwakimbia wanajeshi waliowakamata, walieleza kuwa "walinajisiwa kwa makundi, na walipata majeraha mabaya ya kimwili, na baadhi yao hata walikatwa maziwa." Ukatili huu, kwa kulingana na taarifa za Mkariri wa UM juu ya Haki za Binadamu Alston, ulitukia kwenye sehemu ya Shalio, Kivu Kaskazini katika JKK. Mtetezi wa Haki za Binadamu, aliongeza kusema, operesheni za kijeshi zilioendelezwa bia na vikosi vya ulinzi amani vya UM katika JKK vya MONUC, pamoja na askari wa JKK, zilitekelezwa vibaya, na ziliwapatia waasi wa kundi la FDLR, fursa ya kurejea kwenye vijiji husika, kulipiza kisasi baada ya majeshi ya MONUC na askari wa taifa kukamilisha operesheni zao na kulihama eneo.