Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Usomali inasailiwa tena na Baraza la Usalama

Hali Usomali inasailiwa tena na Baraza la Usalama

Baraza la Usalama asubuhi lilijadilia suala la Usomali kwenye kikao cha hadhara. NKM juu ya Masauala ya Kisiasa, B. Lynn Pascoe na Craig Boyd, ofisa wa Kitengo cha UM Kusaidia vikosi vya Ulinzi Amani vya UA katika Usomali (AMISOM) waliwakilisha ripoti zao kuhusu maendeleo nchini humo.

Pascoe alibainisha kwenye taarifa yake kwamba hali ya usalama Usomali, mnamo miezi michache iliopita, ilikuwa ni ya kigeugeu; na aliongeza kusema licha ya kuwepo wimbi la vurugu nchini, Serikali ya mpito ilisalimika mashambulio ya makundi aliosema yalifadhiliwa silaha nzito nzito kutoka nchi za kigeni. Wakati huo huo, Serikali inaendelea na juhudi za kuitisha mazungumzo ya amani kati yake na yale makundi yalio tayari kuidhinisha mwelekeo huo wa kisiasa. Ofisa wa Kitengo cha Usaidizi cha UM, Craig Boyd, yeye kwenye risala yake alichanganua aina ya misaada inayoipatiwa vikosi vya AMISOM na UM, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha ahadi zilizotolewa mwezi Aprili za kuchangisha dola milioni 200 kuisaidia Usomali zitatekelezwa haraka na wahisani wa kimataifa.