Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon, Ijumatatu, kwenye mkesha wa ufunguzi wa kikao cha 64 cha Baraza Kuu la UM, tarehe 14 Septemba, alijiunga kwenye sala maalumu ya kuomba dua ya mafanikio na amani ulimwenguni. Sala hii kawaida hufanyika kwenye Kanisa la Familia Takatifu (Holy Family Church) kila mwaka kabla ya ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu, ambacho huhudhuriwa na viongozi kutoka nchi zote za dunia na hufanyika kwenye Makao Makuu ya UM kujadiliwa kipamoja miradi ya kuimarisha usalama na amani ya kimataifa. KM alikumbusha kwenye risala yake kwamba wakati UM ukijaribu kuzisaidia nchi maskini kukamilisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), haitoweza kuponesha majeraha ya zile ahli za kimataifa zinazosumbuliwa na shida na matatizo ya kiuchumi. Alitoa mwito maalumu kwa viongozi wote wa makundi ya kidini kujitahidi kuungana ili kuimarisha ule uwezo wa kuyatekeleza malengo ya UM ya kunusuru maisha ya umma, na kuusaidia ulimwengu kuelekea kwenye hali nzuri ya kuusaidia umma, kwa ujumla.

Rashid Khalikov, Mkurugenzi wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Kiutu ya Dharura (OCHA), anakaribia kuhitimisha ziara yake ya siku nne katika Yemen kutathminia hali kwenye maeneo yalioshuhudia mapigano katika wiki za karibuni, na kuchunguza mahitaji hakika ya umma. Alizuru yale maeneo ya Yemen kaskazini ambapo waathirika wa mapigano walipatiwa makazi ya muda. Alipowasili Yemen, mara ya kwanza, Khalikov alinakiliwa akisema ilikuwa ni vigumu, kwa upande wake, kupata sura kamili ya matatizo ya kiutu yaliojiri nchini kwa sababu ya hali ya usalama ya kigeugeu. Mapema mwezi huu, UM ulianzisha kampeni maalumu ya kuomba msaada wa dola milioni 23.7 kwa Yemen, lakini hadi sasa mchango huo bado haujafadhiliwa kutoka wahisani wa kimataifa. Khalikov alisema ana wasiwasi juu ya hali hii, na alkumbusha kwamba Yemen inahitajia haraka msaada wa dharura kutoka wafadhili wa kimataifa kudhibiti haraka hali mbaya ya kimaisha iliopo sasa hivi ili isije ikaharibika zaidi.