Skip to main content

Wakulima wa Zimbabwe wasaidiwa na FAO kuotesha mahindi na mtama

Wakulima wa Zimbabwe wasaidiwa na FAO kuotesha mahindi na mtama

Katika jitihadi za kuisaidia Zimbabwe kukabiliana na tatizo la njaa kwa mwaka huu, Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO), likishirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) yatawapatia mbegu na mbolea baina ya asilimia 10 hadi 15 ya wakulima dhaifu nchini, sawa na wakulima 176,000.

Kila mkulima atafadhiliwa mbegu za mahindi na mtama pamoja na mbolea, ili walime kwa wakati, kabla majira ya kuotesha mbegu hayajaanza mnamo mwisho wa mwezi Septemba. FAO hivi sasa imepokea tani 26,000 za mbegu na mbolea kugawa kwa wakulima wa Zimbabwe, ambapo kila mkulima atapewa vifaa vya kutosha kuotesha mbegu hizo kwenye eneo la 0.5 hekta. Kwa mujibu wa Jean-Claude Urvoy, Mratibu wa FAO juu Miradi ya Dharura katika Zimbabwe "pindi patapatikana mvua za kuridhisha, uratibu wenye nguvu na utekelezaji unaolingana na wakati, kuna uwezekano wa kuzalisha maradufu mavuno ya mahindi na mtama katika mwaka huu, tukilinganisha na mwaka uliopita."