Hapa na pale

Hapa na pale

KM wa UM Ban Ki-moon na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Jean Ping, wametangaza leo kumteua Mohamed Yonis wa Usomali kuwa Naibu Mjumbe Maalumu wa Pamoja kwa Operesheni na Usimamizi wa Kazi za UNAMID katika Darfur. Hivi sasa Yonis ni Mkurugenzi wa Kumudu Shughuli za UNAMID na anatarajiwa kumrithi Hocine Medili wa Algeria ambaye hivi sasa amekamilishi muda wake wa kazi katika Darfur. KM alimshukuru Medili kwa kuitumikia UM kwa miaka thelathini na saba.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti mapigano makali yameshtadi Yemen kaskazini, kwenye jimbo la Sa'ada baina ya vikosi vya Al Houti na majeshi ya Serikali. UNHCR imeeleza kuwa hali ni mbaya zaidi kwenye mji wa Sa'ada, ambao katika wiki mbili zilizopita ulitengwa kwa kila njia. Kwa mujibu wa ripoti za UNHCR mji wa Sa'ada umenyimwa umeme na maji kuanzia tarehe 12 Agosti hadi hivi sasa, na akiba haba ya chakula iliopo inafifia kwa kasi kila siku zikipita. Taarifa za mashirika yanayohudumia misaada ya kihali zinasema hali katika Sa'ada haiwezi tena kudhibitika, hasa kwa zile aila ambazo zimekosa makazi na ambao sasa wamelazimika kukaa na marafiki, jamaa au majirani kwa sababu ya mapigano ya mitaani yaliovuma kwenye maeneo yao. Shirika la Wahamiaji linasema bado halijaweza kufikia jimbo la Al Jawf kuhudumia umma unaokadiriwa 4,000, ambao unahitaji makazi ya muda ya dharura. UNHCR inakadiria watu 150,000 wameathirika na mapigano katika Yemen, ikijumlisha wale wahamiaji wa ndani ya nchi waliokosa makazi.

Ijumaa Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetoa ombi la msaada wa tani za metriki za chakula 217,000 - ambazo zinagharamiwa dola milioni 218 - ili kuhudumia chakula umma muhitaji wa Usomali milioni 3.5 katika mwisho wa Oktoba baada ya akiba iliopo sasa kumalizika. Tangazo la karibuni la WFP limethibitisha kwamba zaidi ya nusu ya raia wa Usomali, sawa na watu milioni 3.8, wanahitajia kufadhiliwa na wahisani wa kimataifa msaada wa chakula ili kuwaepusha na janga hatari la kiutu litakalozuka pindi msaada huo hautopatikana haraka.

Ujumbe wa Ofisi ya Masuala ya Kisiasa kwa Usomali (UNPOS), ulioongozwa na Charles Petrie, Naibu Mjumbe Maalumu wa UM kwa Usomali, wiki hii ulitembelea Somaliland kuchunguza taratibu za kuimarisha shughuli za UM kwenye sehemu hii ya nchi. Wajumbe wa Ofisi ya UNPOS walikutana na wawakilishi wa vyama mbalimbali vya kisiasa, pamoja na wale wanaowakilisha jumuiya za kiraia pamoja na maofisa wengine.