Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Chong Young-jin, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d\'Ivoire amezuru kituo kinachotoa vitambulisho vya wapiga kura katika mji mkuu wa Abidjan. Alisema kazi inayosimamiwa sasa hivi na kituo hiki ni ile ya kukusanya taarifa zilizopokewa za usajili wa wapiga kura na utambulisho. Wiki iliopita Chong alizuru sehemu za bara na maeneo ya ndani ya Cote d\'Ivoire kutathminia hali kwa ujumla.

KM amemteua Jean-Maurice Ripert wa Ufaransa kuwa Mjumbe Maalumu wa Kusimamia Misaada ya Kimataifa kwa Pakistan. Nafasi hii imeanzishwa na KM kuisaidia Serikali ya Pakistan na jumuiya ya kimataifa kukidhi vyema mahitaji ya kiutu, na kufufua uchumi pamoja na ujenzi wa jamii kufuatia mzozo uliosababisha mamia elfu ya watu kung'olewa makazi katika Pakistan. Mjumbe Maalumu mteuzi ataandaa mipango, ya jumla, pamoja na Serikali ya Pakistan na washiriki husika wenzi wa kimataifa, inayohitajika kufufua mahitaji ya kiuchumi na jamii, kwenye yale maeneo yaliaothirika na mizozo ya karibuni. Hivi sasa Ripert analitumikia taifa lake kama ni Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa katika UM, New York.

Ijumatatu, Kai Eide, Mjumbe wa KM kwa Afghanistan ametoa taarifa iliowasihi wagombea uchaguzi, wafuasi wao, na vile vile wapiga kura kuonyesha subira kuhusu matokeo ya uchaguzi nchini mwao, na kuipa fursa Kamisheni ya Kusikiliza Malalamiko ya Uchaguzi kufanya kazi zake na kutoa maamuzi ya lawama walizopokea kwa hivi sasa. Aliyasema haya alipozuru makao makuu ya Kamisheni ya Kusikiliza Malalamiko yaliopo Kabul, ambapo alisisitiza juu ya umuhimu wa kuhishimu utaratibu wa uchaguzi nchini. Alisema anaamini Kamisheni ya Kusikiliza Malalamiko itafanya kila iwezalo, kushughulikia na kurekibisha ukiukaji wa utaratibu uliotukia wakati wa uchaguzi katika Afghanistan.