Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wawasihi viongozi wa dunia kuonyesha vitendo kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa

Vijana wawasihi viongozi wa dunia kuonyesha vitendo kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa

Wajumbe waliohudhuria Mkutano wa Vijana na Watoto wa Kimataifa wa TUNZA, uliofanyika kwenye mji wa Daejeon, Korea ya Kusini walipokamilisha vikao vyao mwisho wa wiki iliopita walitoa mwito maalumu unaowataka viongozi wa dunia kuchukua hatua kali, za dharura, kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ulimwenguni.

Mwito huu ulitolewa baada ya majadiliano ya wiki nane yaliofanyika katika sehemu mbali za dunia, kwa kupitia njia ya mtandao wa kompyuta, majadiliano ambayo yalikamilishwa kwenye Jengo Kuu la Halmashauri ya Jiji la Daejeon, Korea ya Kusini walipokusanyika Vijana na watoto 700, wakiwa na umri wa kuanzia miaka 10 mpaka 24, wakiwakilisha bilioni tatu ya idadi ya watu duniani. Mwito wao ulibainisha kuvunjika moyo na hatua zilizochukuliwa kwa sasa na serikali zao, katika kudhibiti uchafuzi wa hali ya hewa, kwa ujumla. Kwa hivyo, vijana hawa wameamua kutayarisha maandamano katika miji 100, katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, kuwa kama ni mchango mkuu wao katika kuzihamasisha serikali za kimataifa kutimiza ahadi muhimu za kufikia makubaliano ya kuwa na chombo kipya cha kanuni ya kimataifa kitakachotumiwa kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa duniani, hatua ambayo inatarajiwa kukamilishwa kwenye Mkutano ujao wa Copenhagen utakaofanyika baada ya siku 110 zijazo. Mkutano wa Daejeon, Korea Kusini uliandaliwa na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP).