Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Alkhamisi KM alikuwa na mkutano makhsusi na Mjumbe wa Kudumu wa Myanmar katika UM. Kwenye mkutano wao huo KM alimuarifu Mwakilishi wa Myanmar ya kuwa ni matarajio yake, na pia ya jumuiya ya kimataifa, halkadhalika, kwamba Serikali itazingatia, kwa uangalifu mkubwa zaidi, taathira za hukumu watakayotoa kwenye kesi inayomhusu kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi, na anaamini Serikali itatekeleza jukumu lake adhimu la kumtoa kizuizini mapema iwezekanavyo.

KM amelaani, kwa kauli kali kabisa, mashambulio ya maboumu yaliotukia Ijumaa mjini Baghdad, katika misikiti mitano ya wafuasi wa madhehebu ya Ki-Shi'a na kusababisha nusu darzeni ya vifo ikijumuika na majeruhi kadha. KM alisema vitendo vya kushambulia mahali pa ibada haviwezi kuhalalishwa hata kidogo na sababu za aina yoyote, si za kisiasa wala kidini! KM anaamini mashambulio haya yalikusudiwa hasa kuchochea mvutano wa kimadhehebu miongoni mwa raia, na kudhoofisha hali ya utulivu nchini Iraq. Kwa hivyo KM ametoa nasaha kwa umma wa Iraq kutotaharakishwa na tukio hili, na kuwaomba waendelee kuimarisha juhudi za upatanishi kwa kutumia mfumo wa mazungumzo na, hatimaye, kudumisha amani ya taifa lao. Aliongeza kwa kusema UM upo tayari kuusaidia kihakika umma wa Iraq kuyatekeleza malengo hayo.

Ripoti ya nusu mwaka ya Shirika la Usaidizi Amani la UM katika Afghanistan (UNAMA), kuhusu hali ya raia kwenye mazingira ya mapigano, ilielezea kwamba kupanuka kwa mikwaruzano nchini Afghanistan kumezidisha idadi ya vifo vya raia. Ripoti ilitayarishwa na Kitengo cha Haki za Binadamu cha UNAMA na ilisajili ongezeko la vifo vya raia kwa asilimia 24 mnamo miezi sita ya mwanzo ya 2009, tukilinganisha na kipindi hicho hicho katika 2008. Idadi ya raia 1,013 waliuawa katika mwaka huu. Kwa mujibu wa ripoti ya UNAMA baina ya miezi ya Januari hadi Juni 2009, asilimia 59 ya raia waliuawa na makundi yenye kupinga serikali, na wakati huo huo asilimia 30.5 ya raia waliuawa na vile vikosi vinavyounga mkono serikali, hususan yale majeshi yanayoendeleza mashambulio kwa kutumia ndege, hujumu zilizosababisha vifo vya watu 200. Kadhalika, ripoti ilithibitisha watu 400 walijeruhiwa kihorera na makundi yanayopinga serikali, yaliokuwa yakitumia vifaa vinavyoripuliwa kwa mbali, na pia mashambulio ya watu wanaojiua/kujitolea mhanga.

Baraza la UM juu ya Masuala ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) limekamilisha shughuli zake mjini Geneva Ijumaa ya leo na kusimamisha, kwa muda, kikao kinachozingatia masuala ya kimsingi kwa 2009 mpaka wakati ambapo nchi wanachama zitahisi kunahitajika kuitisha kikao kingine cha Baraza katika mwaka huu. Kikao kilichomalizika kilifanyika kwa mwezi mmoja mfululizo, na majadiliano yalilenga yale masuala ya afya ya jamii na mapendekezo kadha yaliwasilishwa na wajumbe wa kimataifa, kwa madhumuni ya kukidhia bora mahitaji ya huduma za afya katika mataifa yanayoendelea. Suala jengine muhimu liliozingatiwa kwenye kikao cha ECOSOC kinaambatana na wasiwasi wa kimataifa kuhusu maamirisho ya utulivu katika yale mataifa yanayoibuka kutoka mazingira ya uhasama na mapigano. Naibu KM kwa Masuala ya Kiuchumi na Jamii, Sha Zukang alisema kwenye hotuba ya kufunga mkutano kwamba Baraza la ECOSOC limethibitisha kidhahiri ni kuwa ndio chombo pekee cha kimataifa chenye uwezo wa kufinyanga na kufuma kipamoja maoni anuwai ya kutoka Mataifa Wanachama kuhusu utekelezaji wa ajenda ya miradi ya maendeleo, kwa ufanisi halisi.