Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Viongozi wa Tume ya Uchunguzi ya UM juu ya mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto imekamilisha ziara yake ya awali katika Pakistan Ijumaa iliopita. Wafanyakazi wa kusimamia shughuli za tume wanatazamiwa kubakia Pakistan kukusanya ushahidi zaidi, na ripoti juu ya uchunguzi wao inatarajiwa kutolewa rasmi kimataifa baada ya miezi sita.

Ripoti ya KM juu ya operesheni za Shirika la Ulinzi Amani katika Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT) imetolewa rasmi Ijumatatu ya leo na imeelezea namna uvamizi, wa muda mfupi wa makundi ya waasi katika mashariki ya Chad, mnamo mwezi Mei, ikichanganyika na mapigano yaliofuatia baadaye baina ya waasi na vikosi vya Serikali yalivyosababisha hali ya usalama katika Chad mashariki kuwa mbaya zaidi. Ripoti ilisema tukio hili liliwapatia majambazi fursa mpya ya kuendeleza vitendo vyao haramu, na kusambaratisha mafanikio yalioletwa na vikosi vya Umoja wa Ulaya (EUFOR) pamoja na taasisi za UM za kurudisha utulivu wa eneo. Vile vile ripoti ilibainisha uhusiano kati ya Serikali za Chad na Sudan uliharibika na kurejesha nyuma usalama wa jimbo zima. KM alisihi Serikali ya Chad na wadau husika wote na mzozo wa taifa kutayarisha mpango wa amani wenye msingi utakaojumuisha makundi yote husika nchini Chad, utaratibu utakaolenga kwenye kiini cha mgogoro ulioselelea Chad mashariki na kujaribu kutafuta suluhu inayoridhisha. Wakati huo huo KM alikumbusha ndani ya ripoti kwamba Shirika la MINURCAT juu ya kuwa linajaribu kuendeleza operesheni zake bila ya vifaa muhimu, hata hivyo jumuiya ya kimataifa inawajibika kulipatia Shirika vifaa inavyohitajia kuimarisha shughuli zake, ikijumlisha helikopta 14 kati ya 18 ilioahidiwa hapo kabla na nchi wanachama, upungufu ambao umesababisha pengo kubwa katika shughuli za usalama. Kwa hivyo, KM ameyahimiza Mataifa Wanachama kuzisaidia nchi zilizojitolea kuchangisha wanajeshi wao kupatiwaa vifaa wanavyovihitajia kikazi na kuwawezesha kuenezwa kulinda amani kwenye maeneo ya mgogoro kama ilivyodhaminiwa na Baraza la Usalama.

Baraza la Uchumi na Jamii (ECOSOC) Ijumatatu limefungua rasmi Geneva majadiliano ya kuzingatia Mada juu ya Masuala ya Kiutu, ambayo yalilenga zaidi kwenye juhudi za kuimarisha ratiba ya kuhudumia misaada ya kihali penye dharura. John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Mshauri wa UM juu ya Misaada ya Dharura, alipohutubia mkutano alikumbusha wajumbe wa kimataifa kwamba maafa yaliojiri ulimwenguni katika 2009 yaliohitajia misaada ya dharura ya kimataifa, yaliangamiza idadi kubwa ya umma. Alisema ile mizozo ilioselelea kwa muda mrefu katika sehemu kadha za dunia iliathiri maisha mamilioni ya umma, mathalan mgogoro wa Darfur, vurugu la katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mashambulio kwenye maeneo ya WaFalastina Yaliokaliwa Kimabavu na pia kuenea kwa hali ya mtafaruku nchini Usomali. Kadhalika, alisema mifumko ya mapigano katika Pakistan, na kumalizika kwa mgogoro wa muda mrefu katika Sri Lanka ni matatizo yaliochafua maisha ya mamia elfu ya watu ziada. Halkadhalika, Holmes alieleza kuwa alisikitishwa sana, na kuzidi kutishwa, na kuongezeka kwa mashambulio dhidi ya wafanyakazi wenye kuhudumia misaada ya kiutu kwenye maeneo yenye mikwaruzano na mapigano. Aliwaomba wajumbe wa Baraza la ECOSOC kujumuika naye katika kulaani, kwa kauli kali, mashambulio haya haramu yasioakubalika na yenye kuhatarisha usalama wa watumishi wenye kuhudumia misaada ya kiutu kwa umma muhitaji.

Timu ya UM Kuratibu na Kutathminia Maafa (UNDAC) leo imeanzisha mafunzo maalumu ya wiki mbili kuwasaidia raia wa Afrika Magharibi na Kati, kupata ujuzi wa kutumiwa kuokoa maisha ya umma pindi hali ya dharura ikijiri kwenye maeneo yao. Mafunzo haya yatapatiwa watu 35 fursa ya kujiunga na familia ya UNDAC baada ya kuhitimu ujuzi maalumu unaohitajika kuokoa maisha ya umma kwenye mazingira ya hatari na maafa. Wajumbe hawa wapya wa UNDAC, hasa kutokea eneo husika la Afrika, watalisaidia eneo lao kuimarisha uwezo wa kudhibiti vyema maafa yatakayozuka katika sehemu za Afrika ya Magharibi na Afrika ya Kati, hasa baada ya kugundulikana maeneo haya siku hizi hayeshi kuvamiwa na maafa ya mara kwa mara. Timu ya Taasisi ya UNDAC ilianzishwa 1993 kwa makusudio ya kuongoza huduma za uokoaji pindi yakizuka maafa ya kimaumbile na kadhalika. Tangu 1993 hadi sasa, wataalamu waliohitimu mafunzo ya UNDAC walishughulikia huduma za kudhibiti hali ya dharura na maafa yaliojiri kwenye nchi 90 ziada ulimwenguni.