Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNMIS ameahidiwa wanajeshi wa Sudan Kusini wataondoshwa kutoka Abyei kungojea maamuzi ya mpaka mpya

Mkuu wa UNMIS ameahidiwa wanajeshi wa Sudan Kusini wataondoshwa kutoka Abyei kungojea maamuzi ya mpaka mpya

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan, Ashraf Qazi ametoa taarifa, leo hii, yenye kueleza kwamba amekaribisha ahadi ziada zilizotolewa na Chama cha NCP na kutoka lile kundi la jeshi la mgambo la SPLM, kuwa watahishimu uamuzi wa Mahakama ya Kudumu juu ya Suluhu ya eneo la mvutano, lenyo mafuta, la Abyei, au Mahakama ya PCA, ambayo inatazamiwa kutangaza uamuzi wa mgogoro wao wa mipaka Ijumatano ijayo.

 Mjumbe wa KM alisema ana wasiwasi na tukio la karibuni ambapo makundi yenye silaha, kutoka Sudan Kusini, yalikiuka makubaliano ya kimataifa kwa kupeleka askari wao kwenye Eneo la Mgogoro la Abyei, wakati uamuzi wa Mahakama ya Upatanishi wa Mipaka kati ya Sudan ya kaskazini na kusini bado haujatolewa. Qazi alisema yeye na maofisa wa UM watakuwepo kwenye eneo la Abyei pale uamuzi wa mipaka mipya utakapotolewa rasmi mnamo kati ya wiki hii. Alisema ameahidiwa vikosi vya Sudan Kusini vimeshachukua hatua za kuwaondosha askari wao kwenye eneo la mgogoro kwa sasa hivi, na amehimiza hali ya eneo hilo inahitajia kudhibitiwa mapema kabla haijazusha mifumo hatari ya fujo na vurugu. Vikosi vya ulinzi amani vya UM kwa Sudan Kusini, kutoka shirika la UNMIS, vimepeleka askari zaidi kwa sasa katika Abyei kulinda raia, pindi patazuka vurugu baada ya Mahakama kutangaza rasmi uamuzi wake wa mipaka wiki hii.