Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon amewatumia viongozi wa Kundi la G-8 barua maalumu, iliyoorodhisha masuala ambayo angelipendelea kuona yanapewa umuhimu kwenye Mkutano Mkuu utakaofanyika mwezi Julai kwenye mji wa l\'Aquila, Utaliana. Aliyataka mataifa yenye maendeleo ya viwandani yaahidi kupunguza kwa kiwango cha baina ya asilimia 25 mpaka 40 vitendo vya kumwaga hewa chafu kwenye anga, itakapofika 2020, kama ilivyopendekezwa na Tume ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (IPCC). Vile vile aliwataka viongozi wa G-8 kuandaa ratiba na utaratibu wa kuchangisha mabilioni ya dola zinazohitajiwa kuyasaidia mataifa dhaifu na masikini kujirekibisha ili kukabiliana na matatizo yaliozushwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika miaka ijayo. Alikumbusha pia kwamba kiwango cha mchango wa kila mwaka unaotakiwa kuyasaidia mataifa ya Afrika kupata uwezo wa kuyakamilisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa wakati, bado ni kidogo sana, chini ya kima cha dola bilioni 20 zilioahidiwa kuchangishwa kwenye Mkutano wa Gleneagles.

 UM umeripoti hali ya usalama katika Darfur kwa sasa ni shwari. Lakini hata hivyo, Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limeyakinisha operesheni zao kwenye eneo bado zinakabiliwa na vitendo vya ujambazi na uharamia, vitendo ambavyo katika siku za karibuni vililenga zaidi Shirika la UNAMID. Kwa mfano, iliripotiwa Ijumatano, nyumba ya watumishi wa UNAMID illibiwa na wezi waliojisaidia vifaa vya elektroniki na fedha. UNAMID inasema itaanzisha haraka uchunguzi juu ya tukio hili. Kadhalika ujambazi uliripotiwa kuzuka kwenye kambi za wahamiaji wa ndani (IDPs) ziliopo kwenye eneo.

Ripoti mpya juu ya Hali ya Madawa ya Kulevya Duniani kwa 2009 iliwakilishwa rasmi leo asubuhi na Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC), kutokea mji mkuu wa Marekani wa Washington D.C. Waraka wa ripoti, wenye kurasa 314, umedhihirisha kwamba biashara ya madawa ya kulevya, ikichanganyika na ile biashara ya bangi na kokeini, kwenye soko la kimataifa haijabadilika sana; lakini inaonyesha dalili za kuteremka, wakati uzalishaji na matumizi ya madawa ya kulevya ya usanisia yameonekana kuongezeka, hasa katika nchi zinazoendelea. Kadhalika ripoti ilisema kuna fungamano halisi kati ya madawa ya kulevya na vitendo vya uhalifu. Antonio Maria Costa, Mkurugenzi Mkuu wa UNODC ametoa mwito wenye kusisitiza uwekezaji mkubwa kwenye huduma za matibabu ya madawa ya kulevya na kwenye shughuli za kudhibiti vitendo vya uhalifu ndio sera zinazotakiwa kutekelezwa ili kudhibiti bora tatizo hili.

KM ameliarifu Baraza Kuu la UM ya kuwa ameamua kuongeza kwa miaka minne zaidi mkataba wa kazi kwa Supachai Panitchpakdi, Mkuu wa Shirika la UM juu ya Maendeleo na Biashara (UNCTAD). Supachai anatarajiwa kuendelea kuendesha kazi za taasisi hiyo kuanzia 01 Septemba 2009 mpaka 31 Agosti 20013.

Kadhalika UNCTAD imeripoti kulitukia mporomoko mkubwa wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, mnamo robo ya mwisho ya 2008, mwelekeo ambao uliselelea vile vile katika 2009. UNCTAD ilisema biashara ya kumiliki na kuwekeza kwenye viwanda vya mataifa jirani, aina ya uwekezaji uliokuwa ukifanyika mara kwa mara katika siku za nyuma, ulianguka kwa asilimia 77 mnamo robo ya kwanza ya 2009 - tukilinganisha na uwekezaji uliofanyika katika mwanzo wa 2008. UNCTAD ilisema uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, kwa ujumla, ulianguka kwa asilimia 54 kimataifa, na iliashiria matarajio yasioridhisha juu ya kufufuka kwa kadhia hii, kuanzia kipindi cha sasa hadi mwisho wa mwaka.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) limeripoti kiashirio kipya cha kupima mradi wa malipo ya bima kitaanza kutumiwa kuwasaidia wakulima, wachungaji na wavuvi katika mataifa yanayoendelea. Kwa mujibu wa UNDP, mpango huu wa bima ni utaratibu mbadala wa sera za bima, kwa sababu mradi huu mpya utazingatia pia mabadiliko ya hali ya hewa inapoashiria malipo, kwa kuzingatia, mathalan, kama mvua zilikuwa haba au la.