Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la Nzige Wekundu ladhibitiwa Afrika Mashariki: FAO

Janga la Nzige Wekundu ladhibitiwa Afrika Mashariki: FAO

Juhudi za dharura, zinazoungwa mkono na UM, kudhibiti bora tatizo la kuripuka janga la Nzige Wekundu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimeripotiwa karibuni kufanikiwa kuwanusuru kimaisha mamilioni ya wakulima, baada ya kutumiwa, kwa kiwango kikubwa, ule utaratibu wa kuangamiza kianuwai vijidudu hivi vinavyokiuka mipaka na kuendeleza uharibifu wa kilimo pamoja na kuzusha njaa.

Huduma ya kuwaangamiza Nzige Wekundu iliendelezwa bia na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) na Shirika la Kimataifa Kudhibiti Nzige Wekundu Kusini na Afrika ya Kati (IRLCO-CSA) katika sehemu tatu za Tanzania: kwenye Mbuga ya Taifa ya Iku-Katavi, nyanda za Ziwa Rukwa na Bonde la Mto Malagarasi. Kwa mujibu wa taarifa ya FAO, pindi Nzige Wekundu watashindwa kudhibitiwa mapema, kuna hatari ya mabumba ya wadudu hawa kuruka kwenye eneo kubwa la ardhi ya kilimo na kuteketeza mavuno ya nafaka, miwa na mazao mengine ambayo mara nyingi huoteshwa na wakulima wadogo wadogo. Taarifa za FAO zinakadiria Nzige Mwekundu aliyepevuka hula gramu mbili ya chakula kibichi katika kila saa 24 - sawa na uzito wa nzige mmoja. Kadhalika, ripoti ilibainisha kwamba jumla ya chakula kinacholiwa na kundi wastani la Nzige Wekundu, kwa siku moja, ni sawa ya jumla ya chakula kinachotumiwa kila siku na watu 2,500.