Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano mkuu wa UM juu ya athari za mizozo ya Uchumi na Kifedha Duniani waanza rasmi makao makuu

Mkutano mkuu wa UM juu ya athari za mizozo ya Uchumi na Kifedha Duniani waanza rasmi makao makuu

Baraza Kuu la UM limeanzisha rasmi, Ijumatano ya leo, Mkutano Muhimu juu ya Mzozo wa Uchumi na Fedha Duniani na Athari Zake Kwenye Huduma za Maendeleo ambao utafanyika kwa siku tatu kwenye Makao Makuu ya UM yaliopo mjini New York.

Kikao hiki cha wawakilishi wote kitatathminia mporomoko mkubwa wa uchumi wa kimataifa, uliozuka karibuni, hali ambayo mara ya mwisho ilishuhudiwa ulimwenguni katika miaka ya 1930. Raisi wa Baraza Kuu, Miguel d'Escoto Brockmann, kwenye hotuba yake ya ufunguzi alisema Mataifa Wanachama yamebarikiwa sasa hivi na "fursa ya kihistoria - na majukumu ya pamoja - ya kuwakilisha utulivu mpya, na unaosarifika, kwenye mifumo ya uchumi na kifedha katika dunia." Kadhalika, KM Ban Ki-moon, kwa upande wake, aliwahimiza wajumbe waliohudhuria mkutano kushirikiana kipamoja kurekibisha huduma za uchumi na fedha, kwenye soko la kimataifa, ili kuhakikisha "zinalingana na mahitaji ya umma kwa karne ya 21." Wajumbe kutoka Mataifa Wanachama 140 ziada wanahudhuria kikao hiki, ikijumlisha nchi tajiri na zile zinazoendelea. Mkutano juu ya Athari za Mzozo wa Kiuchumi na Fedha Duniani unatazamiwa kuyapatia mataifa masikini jukwaa la kuwakilisha sauti zao katika kukabiliana na matatizo husika, hasa ilivyokuwa mataifa haya ndio yalioathirika zaidi na mporomoko wa uchumi wa dunia. Tutakupatieni ripoti zaidi baadaye.