Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM atoa mwito wa kuzikomesha chuki za kwenye uwanda wa intaneti

KM atoa mwito wa kuzikomesha chuki za kwenye uwanda wa intaneti

Ijumanne, kwa siku nzima mfululizo, Idara ya Habari ya UM kwa Umma (DPI) ilifanyisha warsha maalumu kuzingatia taratibu za kusitisha zile kurasa za mitandao ya kompyuta zenye kuchochea chuki.

Kaulimbiu ya warsha inasema "Chuki za Mitandao: Zahatarisha Uwanda wa Mtandao". KM alikiri kwenye risala ya ufunguzi ya kuwa mtandao wa intaneti ulituwasilishia mengi mazuri na pia kurekibisha maisha ya wanadamu na kuleta mageuzi kuhusu nidhamu za namna ya kufanya kazi. Lakini teknolojiya hiyo, alitanabahisha KM, vile vle imetuletea maovu yaliojizatiti kwenye vichochoro vya giza liliotanda totoro kwenye uwanda wa mawasiliano ya kisasa, ambapo kumekutikana baadhi ya watu waliokakamaa kuendeleza teknolojiya ya mawasiliano yenye kuimarisha mawazo ya kibaguzi, na kueneza taarifa mbaya za kupotosha na kueneza chuki. Alikumbusha KM mawazo kama hayo ni hatari kitaaluma, hususan kwa vijana wenye kuvutika kirahisi na walionyimwa maoni ya kukosoa. Aliwaomba wazee, makampuni ya Intaneti/Wavuti, wabuni sera pamoja na wadau wengineo kuchangisha msaada wao na kukomesha mawasiliano ya chuki na udhalimu unaopaliliwa kwenye mitandao ya kompyuta na katika mifumo mengine ya mawasiliano ya teknolojiya ya kisasa.