Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Kimataifa kwa Mtoto wa Afrika

Siku ya Kimataifa kwa Mtoto wa Afrika

Tarehe ya leo, Juni 16, inaadhimishwa na UM kuwa ni "Siku ya Kimataifa kwa Mtoto wa Afrika." Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limetangaza ya kuwa kuna baadhi ya nchi katika Afrika, zilizoonyesha maendeleo makubwa ya kutia moyo, kwenye zile juhudi za kuhudumia watoto wachanga kuishi.

Mathalan, UNICEF ilithibitisha kwamba vifo vinavyotokana na maradhi ya shurua katika nchi za Afrika ziliopo kusini ya Jangwa la Sahara, viliteremka kwa asilimia 89 katika kipindi cha baina ya 2000 na 2007, kwa sababu ya juhudi za pamoja kati ya serikali husika na mashirika wenzi ya kimataifa, katika kuwapatia watoto wachanga chanjo dhidi ya shurua. UM inasema ijapokuwa nusu ya vifo vya watoto milioni 9.2 katika dunia, walio chini ya umri wa miaka mitano, hutukia zaidi katika bara la Afrika, hata hivyo, kuanzia 1990, baadhi ya mataifa masikini barani humo, kama Eritrea, Ethiopia, Malawi na Niger - yalifanikiwa pia kupunguza, takriban kwa asilimia 40, vifo vinavyosababishwa na shurua vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano.