Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon ametangaza taarifa yenye kulaumu vikali shambulio la bomu liliofanyika katika mji wa Lahore, Pakistan, ambapo watu 30 ziada waliripotiwa kuuawa na 250 wengine walijeruhiwa. Alisema hakuna kitendo chochote kinachohalalisha kosa hili la vurugu inayochochewa na ugaidi. KM aliwatumia mkono wa taazia aila za waathirika wa tukio hilo, na kuwaombea majeruhi wapone haraka, na kukukumbusha ushikamano uliopo baina yake na Serikali, pamoja na umma wa Pakistan, kwenye zile juhudi za kuwafikisha waliondeleza makosa haya mahakamani kukabili haki.

 Luc Chauvin, naibu Mwakilishi wa UNICEF kwa Pakistan ameripoti jumla ya watu waliong'olewa makazi kwa sasa, kutokana na mapigano katika Jimbo la Mpakani la Kaskazini Magharibi (NWFP) imefikia wahamiaji milioni tatu. Aliiambia Redio ya UM umma huu uliokosa makazi unaendelea kukabiliwa na maafa ya kihali, na aliisihi jumuiya ya kimataifa kutopwelewa kwenye zile jitihadi za kuchangisha misaada ya dharura ya fedha inayotakikana kunusuru maisha ya mamia elfu ya waathirika wa mapigano katika Pakistan. Alisema tangu UM na wahudumia misaada ya kiutu kutoa ombi la kuchangisha msaada wa dharura wa dola milioni 543, zinazohitajika kuhudumia kihali raia waliong'olewa makazi, kufuatia mashambulio ya vikosi vya Serikali ya Pakistan dhidi ya makundi yenye siasa kali, jamii ya kimataifa ilifanikiwa kupokea dola milioni 88 tu, sawa na asilimia 16 ya maombi. Wakati huo huo, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) imeeleza kuwa ni asilimia 10 tu ya watu waliongo'lewa makazi wanaoishi kwenye kambi zinazohudumiwa na mashirika ya kimataifa. Jumla iliobaki, yaani asilimia 90 ya wahamiaji, UNHCR ilisema wanaishi na marafiki, jamaa, au kwenye majengo ya jamii, kama vile maskuli na kadhalika. Hata hivyo, UNHCR imeeleza kuwa itaendelea kuwahudumia misaada ya kiutu wahamiaji wote, waliopo kwenye kambi za UM na wale nje ya maeneo hayo.

Imeripotiwa na Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) kwamba tangu KM Ban Ki-moon kumaliza ziara ya Sri Lanka, mnamo wiki iliopita, magari ya mashirika yenye kuhudumia misaada ya kiutu yaliruhusiwa, kwa muda kuingia na kutoka kwenye maeneo ya Mashamba ya Menik kupelekea misaada kwa waathirika wa mapigano; lakini hayatoruhusiwa kutumia bendera za mashirika ya kimataifa wala kushindikizwa na ulinzi. Kadhalika OCHA imearifiwa ya kuwa vikosi vya Sri Lanka vitahamishwa kutoka zile kambi za raia waliokosa makazi, na majukumu ya kuendesha shughuli za kambi hizo yatakabidhiwa watumishi raia. Wakati huo huo OCHA ilisema mahitaji ya jumla ya katika kambi za wahamiaji yamefikia kiwango cha hatari, na kuna haja kuu ya kutuma misaada ya dharura kukidhi mahitaji ya vituo vya afya, madaktari na wahudumia afya pamoja na maji safi na mazingira ya usafi, halkadhalika.

Ijumanne, Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva limehitimisha majadiliano ya Kikao Maalumu cha 11 kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu katika Sri Lanka, na kupitisha azimio liliohimiza Serikali kuendeleza shughuli zake kwa utaratibu utakaohakikisha makabila yalio wachache nchini hayatobaguliwa. Vile vile azimio la Baraza la Haki za Binadamu limependekeza kuwepo ushirikiano kati ya jumuiya ya kimataifa na Serikali ya Sri Lanka kwenye zile juhudi za kufufua huduma za kiuchumi na jamii nchini baada ya mapigano kusitishwa, na pia kuyataka Mataifa Wanachama kuongeza mchango ziada wa fedha kuyatekeleza hayo. Azimio lilipitishwa kwa kura 29 na nchi 12 zilipiga kura ya upinzani, wakati mataifa 6 kutopiga kura.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetangaza ripoti mpya kuhusu vikwazo dhidi ya uhuru wa mtu kutembea atakapo kwenye eneo liliokaliwa kimabavu la WaFalastina katika Magharibi ya Ufukwe wa Mto Jordan. Ripoti iliyakinisha kwamba hatua kadha zinazochukuliwa na Israel ni mbinu zinazotumiwa kuongeza vikwazo dhidi ya haki ya raia wa KiFalastina kutembea watakapo, mathalan, upanuzi wa vituo vya ukaguzi na ujenzi wa barabara mbadala za chini kwa chini ya ardhi. Taathira za maamuzi haya ya Israel, ripoti ilitilia mkazo, husababisha WaFalastina kupoteza ardhi ya jadi na kuvuruga uwezo wao wa kutumia njia za kawaida, na huku umegaji haramu wa ardhi zao ukiendelea. Kwa mujibu wa ripoti makazi ya walowezi wa Israel katika eneo hili ndio vipengele hakika vyenye kuchochea vikwazo dhidi ya uhuru wa mtu kwenda atakapo.

KM ameliarifu Baraza la Usalama kwamba ameazimu kumteua Sahle-Work Zewde wa Ethiopia kuwa Mjumbe Maalumu na pia Mkuu wa Ofisi ya Ujenzi Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (BONUCA), ofisi ambayo itabadilishwa rasmi jina baadaye na kuwa Ofisi ya Mchanganyiko juu ya Huduma za Ujenzi Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (BINUCA). Bi Zewde ni mwanamke wa pili anayewakilisha wadhifa wa Mjumbe Maalumu wa KM chini ya Ban Ki-moon, na atachukua nafasi ya François Fall baada ya kumaliza mkataba wake wa kazi.

Kadhalika, Robert Watkins wa kutoka Kanada, ameteuliwa na KM kuwa Naibu Mjumbe Maalumu kwa Afghanistan na anatarajiwa pia kutumika kama Mratibu Mkaazi wa UM na Mratibu wa Misaada ya Kiutu katika Afghanistan. Atachukua nafasi ya Bo Asplund wa Uswidin atakapomaliza muda wa kazi katika wakati wa kiangazi mwaka huu.