Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Adhuhuri Baraza Kuu la UM lilipigisha kura maalumu ya kuchagua wanachama 18 wa kutumikia Baraza la UM juu ya Haki za Bindamu, kwa muda wa miaka mitatu ijayo kuanzia tarehe 18 Juni 2009. Miongoni mwa Mataifa Wanachama yaliochaguliwa kuwakilishwa kwenye Baraza kwa mara ya kwanza inajumlisha Ubelgiji, Hungary, Kyrgyzstan, Norway na Marekani. Baraza la Haki za Binadamu lina wajumbe 47 na lilianzishwa 2006 baada ya Kamisheni ya Haki za Binadamu kusitishwa kazi, kwa sababu ya madai ya baadhi ya mataifa kwamba Kamisheni hii ilikuwa haina nguvu ya kutekeleza madaraka ya kazi, na shughuli zake zilikuwa haziridhishi mataifa fulani ambayo yalidai pia Kamisheni ilikosa uwajibikaji kwenye maamuzi yake. Mataifa yafuatayo pia yalichaguliwa kwa mara ya pili kutumikia Baraza la Haki za Binadamu: Bangladesh, Cameroon, Uchina, Cuba, Djibouti, Jordan, Mauritius, Mexico pamoja na Nigeria, Urusi, Senegal na Uruguay.

Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur, Rodolphe Adada leo alikuwa na mazungumzo maalumu mjini Kahrtoum na Mutrif Siddiq, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan, na pia alikutana na Mshauri wa Raisi, Mustafa Osman Ismail ambao aliwaelezea wasiwasi alionao juu ya amani ya eneo baada ya kufumka mapigano miongoni mwa makundi yanayohasimiana katika Um Baru, Darfur Kaskazini. Shirika la Ulinzi Amani la UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limechukua jukumu la kuwahamisha watu waliojeruhiwa kwenye mapigano na kuwapeleka kupata matibabu. UNAMID ilitoa mwito unayotaka uhasama usitishwe haraka na kuyataka makundi yanayohasimiana yajiunge kwenye miradi ya kurudisha amani, badala yake.

Ijumatatu alasiri Baraza la Usalama lilihitimisha mkutano wa mawaziri uliozingatia hali ya usalama katika Mashariki ya Kati, na kupitisha Tamko la Raisi wa Baraza liliohimiza kufufuliwa haraka zile juhudi za dharura zinazotakiwa kufikia amani ya kudumu, miongoni mwa makundi husika na mgogoro pamoja na jumuiya ya kimataifa. Juhudi hizi zilitakiwa zichangishe mfumo wa jumla wa amani, ulio wa haki na utakaoweza kudumishwa katika Mashariki ya Kati. Baraza limesisitiza, kwa mara ya pili, kwamba linaunga mkono mtazamo wa kuwepo Mataifa mawili jirani ya kidemokrasia katika Mashariki ya Kati, yaani Izraili na Falastina, yatakayoishi pamoja kwa amani ndani ya mipaka inayotambulika kisheria kimataifa. Baraza la Usalama limeunga mkono pia pendekezo la Shirikisho la Urusi la kuitisha mkutano wa kimataifa Moscow 2009 kuzingatia amani ya Mashariki ya Kati, baada ya kushauriana Wapatanishi wa Pande Nne pamoja na yale makundi yanayohusika na mgogoro huo.

Matokeo ya ripoti ya utafiti mpya wa Shirika la UM juu ya Haki ya Wafanyakazi wa Kimataifa (ILO) imebainisha kwamba dola bilioni 20 hupotea kila mwaka duniani kwa sababu ya vibarua vya kulazimisha. Ripoti imeorodhesha vitendo haramu vinavyoendelea kukithiri, vinavyosababisha mtu kushiriki kwenye ajira ya lazima, mizungu ambayo husababishwa na desturi zisio na maadili, za ulaghai na za kihalifu. Ripoti imetoa mwito maalumu wa kukuza kipamoja juhudi za kuzikomesha tabia hizi karaha. Kadhalika ripoti ya ILO imezingatia maendeleo yaliofikiwa hadi sasa kwenye juhudi za kimataifa za kupunguza na kuzuia kazi ya kulazimisha. ILO imeonya ajira ya lazima inahitajika kidhibitiwa au si hivyo itazalisha athari hasi kijumla kwenye uchumi wa dunia na kupalilia zaidi migogoro ya kuzalisha ajira.

Shirika la UM juu ya Maendeleo na Biashara (UNCTAD) limetoa mwito unaohimiza jumuiya ya kimataifa kuzipatia nchi zinazoendelea hifadhi bora na uwezo wa kushiriki kwenye biashara ya kimataifa, hasa katika kipindi ambapo tumekabiliwa na mgogoro hanikiza wa fedha duniani. UNCTAD inasisisitiza kadhia hii ikitekelezwa itazisaidia nchi masikini kutumia bidhaa zao zinazosafirishwa nje kufufua uchumi wa kizalendo. Kwenye majadiliano ya Mkutano wa UNCTAD uliofanyika Ijumatatu, KM wa taasisi hiyo, Supachai Panitchpaki alitilia mkazo kwenye risala yake kwamba vifurushi vya misaada inayofadhiliwa nchi tajiri na serikali zao kufufua uchumi ulioselelea kwenye maeneo yao, ni lazima vitumiwe kwa utaratibu utakaohakikisha huchochea mahitaji ya bidhaa kwenye soko la kimataifa. Alitahdharisha kwamba ishara za uchumi kufufuka kwenye mataifa yenye maendeleo ya viwandani, zilizoibuka karibuni, zisiwahadae wabuni sera kudhania mzozo wa kiuchumi unakaribia kumalizika duniani, na ilhali kuna kila dalili mgogoro huu utaendelea kuselelea kwa usugu usiotarajiwa katika maeneo mengineyo ya ulimwengu.

Mataifa Yalioridhia Mkataba wa UM juu ya Sheria ya Bahari wameekewa muda maalumu, mpaka saa sita za usiku, Ijumanne ya leo, kuwasilisha kwa ile Kamisheni ya Mipaka ya Uketo wa Bahari, kwa kupitia KM eneo rasmi la mamlaka ya kisheria ya mipaka yao ya bahari. Mkataba ulioidhinishwa na kuwa chombo cha sheria ya kimataifa 1994 ndio unaobainisha mfumo wa haki na dhamana ya Mataifa Yalioridhia Mkataba juu ya matumizi ya utajiri uliopo katika bahari za dunia. Vifungu vyengine vya Makataba vimeidhinisha mipaka halisi kisheria inayoruhusiwa kuwa kwenye mamlaka ya taifa, ikijumlisha maili 12 za eneo la bahari pamoja na maili 200 liliotengwa pekee kwa shughuli za uchumi. Mpaka sasa mataifa 157 pamoja na Umoja wa Jamii ya Ulaya yamejiunga na Mkataba wa UM wa Sheria ya Bahari.