Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) ametoa mwito maalumu uliohimiza ushirikiano wa kimataifa kwenye juhudi za kuwasaidia kihali mamia elfu ya raia wa Pakistan waliong\'olewa makazi kwa sababu ya mapigano yaliozuka karibuni. Alieleza kwamba UNHCR, kwa upande wake, imeshaanza kupeleka misafara ya ndege zilizobeba misaada ya kiutu, ili kukidhi mahitaji ya dharura kwa umma uliopo kwenye eneo la uhasama la kaskazini-magharibi katika Pakistan. Guterres alisisitiza idadi kubwa ya umma unaomiminikia kwa kasi kwenye eneo la mapigano unahitajia misaada ya kihali haraka ili kunusuru maisha.

Shirika la UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) limeripoti vikosi vya ulinzi vya Serikali vya Sri Lanka vinaendelea na operesheni zake za kijeshi dhidi ya wapinzani, kwenye eneo la ugomvi na mikwaruzano. Mapigano makali yaliripotiwa kuzuka mwisho wa wiki yaliosababisha vifo vya mamia ya raia na mamia ya majeruhi. Iliripotiwa mapema Ijumatatu raia 900 waliwasili Omanthai kutoka sehemu ya mapigano ya Mullaitivu. Jumla ya watu 196,044 kutokea mazingira ya mapigano wameweza kuingia kwenye eneo liliodhibitiwa na Serikali kwa hivi sasa. Hata hivyo, UM unakadiria watu 50,000 ziada bado wamenaswa kwenye maeneo ya mapambano.

Shirika la Usaidizi Amani la UM katika Afghanistan (UNAMA) limearifu kuingiwa moyo na uteuzi wa idadi kubwa ya wanawake watakaogombania uchaguzi ujao wa halmashauri za majimbo nchini, jumla ambayo imekiuka uchaguzi uliopita kwa wagombea 20 zaidi. Kamisheni Huru ya Kusimamia Uchaguzi Afghanistan imeiarifu UNAMA wagombea uchaguzi 3,324 wamesajiliwa rasmi kushiriki kwenye uchaguzi wa majimbo, ikijumlisha wanawake 342, hatua inayomaanisha wanawake watajihusisha kihakika kwenye juhudi za kuongoza maendeleo ya taifa lao kwa wakati ujao.

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) amelaumu, kwa lugha kali, uvamizi wa jinai ulioendelezwa na waasi wa Rwanda katika usiku wa tarehe 08 Mei (09) kwenye kijiji cha kaskazini-mashariki cha Butolonga. Doss alisema mashambulio haya yanathibitisha wazi, kwa mara nyengine tena, ya kwamba waasi walioendeleza mashambulio wa kundi la FDLR ni "majambazi" halisi. Kwa mujibu wa ripoti za Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC), waasi wa FDLR walipovamia kijiji cha Butolonga walishambulia kwa marisasi, na kuua askari wawili wa Kongo, na pia kuchoma moto nyumba 131. Baada ya tukio hili, walinzi wa amani wa UM waliopelekwa kwa uchunguzi, walikikuta kijiji kitupu kwa sababu wanakijiji wote walikimbia vichakani kutafuta usalama, wakazi ambao inaripotiwa hivi sasa wameonekena kuanza kurejea makwao.

Taarifa ya tarehe 11 Mei 2009 ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu hali ya maambukizi ya homa ya mafua ya A(H1N1) ulimwenguni imehakikisha rasmi wagonjwa 4,694 waliripotiwa kupatwa na vimelea vya maradhi - tukilinganisha na wagonjwa 2,500 wa maradhi walioripotiwa na WHO Ijumaa ya tarehe 08 Mei (2009) kuambukizwa na maradhi, ikijumlisha pia vifo 53. WHO imearifu pia nchi 30 zimethibtisha kuwepo wagonjwa wa homa ya mafua ya H1N1 kwenye maeneo yao - tukilinganisha na nchi 25 zilizoripoti maradhi haya wiki iliopita. Hata hivyo, kiwango cha ilani ya hadhari ya maambukizi ya maradhi kimataifa bado kimesalia kwenye rakamu ya tano, kwa kuambatana na ushauri wa WHO.

Kuanzia tarehe 11 mpaka 14 Mei Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) linafanyisha mkutano maalumu Geneva kuzingatia hali ya uhusiano wa ajira kwenye viwanda vya kutengenezea petroli, hasa kwenye mazingira ya ulimwengu unaoshuhudia upungufu mkubwa wa ajira katika sekta ya mafuta na gesi. Majadiliano ya mkutano yanatazamiwa kupitisha mapendekezo kadha wa kadha yatakayojumlisha pia maazimio yanayohusu taratibu za kuimarisha shughuli zinazosarifika za biashara ya nishati, pamoja na huduma zitakazozalisha ajira inayohishimika kwa mfanyakazi. Mkutano wa ILO umekusanyisha wajumbe mbalimbali wa kimataifa waliowakilisha serikali, mashirika ya wafanyakazi na wajasiriamali wa kimataifa.

Shirika la Utalii Duniani (WTO) limemteua Taleb Rifai kuwa Katibu Mkuu wake mpya. Rifai aliyekuwa Waziri wa Utalii Jordan anatarajiwa kuanza kazi Januari 2010, baada ya uteuzi wake kuidhinishwa na Baraza Kuu la WTO, litakapokutana Kazakhstan katika wiki ya mwanzo ya Oktoba. Tangu mwezi Machi Rifai alishika wadhifa wa KM wa muda wa WTO, na kabla ya hapo, kuanzia 2006, alikuwa Naibu KM wa shirika hilo la utalii.