Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makisio ya UM kuhusu hali katika jimbo la NWFP, Pakistan

Makisio ya UM kuhusu hali katika jimbo la NWFP, Pakistan

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti hali kwenye eneo la mapigano la Jimbo la Mpakani Pakistan katika Kaskazini-Magharibi (NWFP) inashuhudia muongezeko mkubwa wa mateso kwa raia walionaswa katikati ya mapigano.

Mashirika yanayowakilisha jumuiya zinazohusika na ugawaji wa misaada ya kiutu Pakistan kwa sasa zinahudumia kihali  wahamiaji wa ndani ya nchi 556,539. Wahamiaji 93,000 kati ya jumla hiyo wamewekwa kwenye kambi za makazi ya muda kwenye Jimbo la Mpakani Pakistan. OCHA imeripoti kuwa na wasiwasi juu ya usalama wa raia waathirika, kwa sababu ya mashambulio ya pande zote mbili zinazohasimiana, hususan baada ya miundombinu ya eneo kuharibiwa, kama vile mabarabara na madaraja. Ripoti za Shirika la UM juu ya Wahamiaji (UNHCR) zimeeleza kwamba jumla ya wahamiaji waliosajiliwa rasmi kuhitajia misaada ya kiutu na mashirika ya kimataifa imekiuka 500,000 ziada. Ndege za UNHCR hivi sasa zinapeleka kwenye kambi za wahamiaji misaada ya vyandarua, makoroja ya plastiki yanayotumiwa kuekeza vibanda vya dharura na pia vifaa vyengine vya kihali, vifaa ambavyo husafirishwa kutoka ghala za UM ziliopo Dubai; vifaa hivi vinapelekwa kwenye Jimbo la Mpakani Pakistan. Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) nalo vile vile limeanzisha vituo 15 vya kugawa misaada ya dharura kwa waathirika wanaokadiriwa milioni 1.5 katika miezi miwili-mitatu ijayo. Halkadhalika, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetuma timu maalumu ya ukaguzi, ya wataalamu watatu, watakaofanya tathmini ya mahitaji ya afya kwenye eneo la mgogoro la Pakistan, baada ya kupokea msaada wa dharura kutoka Mfuko wa UM wa Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF kwa lengo la kuimarisha huduma za kufarajia afya.