Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Naibu Katibu Mkuu (NKM) wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro amewasili Pretoria kumwakilisha KM kwenye taadhima za Ijumamosi za kuapishwa kwa Raisi mteule wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Atakapokuwepo huko NKM Asha-Rose atafanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi wa Afrika Kusini na wale wanaowakilisha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) – kuzingatia zaidi masuala ya amani, maendeleo ya kiuchumi, pamoja na kusailia hitimisho la mashauriano yao kuhusu kikao Mkutano Mkuu wa Copenhagen juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani utakaofanyika mwisho wa mwaka.

Dmitry Titov, KM Mwandamizi juu ya Sheria na Taasisi za Usalama kwenye Idara ya Operesheni za Amani za UM (DPKO) Ijumaa asubuhi aliwakilisha taarifa maalumu mbele ya kikao cha hadhara cha Baraza la Usalama kilichosailia mapigano yaliozuka Chad mashariki wiki za karibuni. Titov aliripoti Shirika la Ulinzi Amani la UM kwa Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT) limethibitisha kihakika kwamba Jeshi la Taifa la Chad lilmeshadidi kuongoza mashambulio ya anga dhidi ya safu za wapiganaji waasi katika eneo la Goz Beida, Chad mashariki.

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limeripoti kuuawa askari wake mmoja Alklhamisi (07/05/2009) usiku katika Darfur Kusini. Ripoti ilisema mnamo saa 2:30 usiku, majambazi wasiotambulikana walimpiga risasi mwangalizi wa kijeshi wa UNAMID alipokuwa anafungua mlango wa nyumba yake iliopo Nyala, mji mkuu wa jimbo, kwa madhumuni ya kuegesha gari. Aliharakishwa kupelekwa hospitali kwa matibabu na watumishi wa UNAMID lakini alifariki alipofika huko. UNAMID imeripoti tukio hili kwa maofisa wa serikali ya kienyeji, pamoja na polisi wa Serikali na watu wa usalama wa taifa, ambao wamejumuika kuendeleza uchunguzi wa tukio. Baadaye gari ya askari aliyeuliwa lilikutikana limetupwa kilomita saba kutoka Nyala. Mwanajeshi wa UNAMID ni wa 15 kuuawa tangu kuanzishwa shughuli za amani Darfur mnamo mwanzo wa 2008. Rodolphe Adada, Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UM/UA kwa Darfur, amelaani vikali mauaji haya, na alitilia mkazo kwamba mashambulizi dhidi ya walinzi amani ni sawa na kosa la jinai ya vita.

Tume ya Kuchunguza Ukweli, ilioanzishwa rasmi mwezi uliopita na Baraza la Haki za Binadamu kuchunguza uharamishaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa sheria za kiutu, kufungamana na mzozo wa karibuni kwenye eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza, wiki hii imeanza rasmi kazi zake Geneva. Tume inajumlisha wajumbe wanne, wakiongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini na walikutana na wadau husika mbalimbali, ikijumuisha wawakilishi wa Mataifa Wanachama, watumishi wa UM na wale wa mashirika yasio ya kiserikali. Vile vile Tume imetayarisha hadidu rejea pamoja na ratiba ya miezi mitatu ya kazi. Wajumbe wa Tume ya Kuchunguza Ukweli katika Ghaza inatazamiwa baadaye kuzuru maeneo yaliodhurika na mapigano, ikijumuisha Israel kusini na vile vile yale Maeneo Yaliokaliwa Kimabavu ya WaFalastina, ikijumlisha Tarafa ya Ghaza. Wenye madaraka Israel walitakiwa washirikiane kikamilifu na kazi za Tume.

Mashirika ya UM, yakishirikiana na Benki Kuu ya Dunia yametangaza kuwa yatashirikiana kujenga vijiji maalumu Burundi, vitakavyojulikana kama ‘vijiji vya amani' ambapo watawekwa raia waliokimbia makwao wakati wa mapigano na wasiomiliki ardhi, pamoja na raia masikini waliopokonywa mali zao. Maeneo haya yatajulikana kama Vijiji vya Muungano (RIV); na kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) vijiji 11 vitajengwa kwenye majimbo ya kusini mwaka huu.

Watoto 750,000 wa chini ya umri wa miaka mitano katika Usomali pamoja na wanawake wenye umri wa kuzaa 500,000 wanahusishwa kwenye kampeni maalumu ya afya na UNICEF, iliokusudiwa kuwapatia chanjo kinga dhidi ya maradhi kadha wa kadha, mradi utakaowafadhilia pia vitamini A pamoja na vifaa vya kujikinga na maradhi ya kuharisha na kudhibiti uigonjwa wa minyoo ikichanganyika na miradi kadha mwengineyo ya kudhibiti afya bora.