Hapa na pale

1 Aprili 2009

KM Ban Ki-moon amewasili London leo hii kuhudhuria mkutano mkuu wa mataifa wanachama wa kundi la G-20.

Alkhamisi KM atahutubia viongozi wa kundi la G-20 wanaowakilisha mataifa yenye uchumi mkuu, ambapo anatarajiwa kuwahadharisha kwamba ni muhimu kuukomesha mgogoro wa uchumi uliotanda ulimwenguni sasa hivi, na kuhakikisha wanashirikiana kwenye harakati za kufufua uchumi wa kimataifa, kijumla, au si hivyo kuna hatari ya janga kuu la kiutu kupamba ulimwenguni. Hatua za pamoja zinatakikana kuimarisha maendeleo, anaamini KM, hali ambayo ikikamilishwa itaupatia umma matumaini juu ya maisha ya siku zijazo.

Mratibu wa Misaada ya Kiutu kwa eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza amewasilisha ripoti mpya inayoonyesha mnamo wiki iliomalizikia tarehe 28 Machi 2009, malori 721 ya bidhaa yaliruhusiwa na serikali ya Israel kuingia kwenye eneo. Ofisi ya UM inayohusika na Misaada ya dharura (OCHA) imeeleza kwamba vikwazo vilivyowekwa na Israel dhidi ya uingizaji na usafirishaji wa bidhaa katika Ghaza ni hali inayoendelea kuathiri vibaya sana kimaisha umma. Idadi kubwa ya wakazi wa Ghaza hutegemea mazao ya karibuni kwa chakula na kuishi. Ripoti pia imebainisha kupigwa marufuku kuingizwa Ghaza wiki hii vifaa vya ujenzi, zana za viwanda, wanyama wa kufuga, mafuta ya petroli pamoja na nishati ya dizeli. Hali kadhalika watu 35,000 wamenyimwa uwezo wa kupata maji safi na salama katika Ghaza, wakati wagonjwa wanaohitajia kupata matibabu nje ya eneo liliokaliwa kimabavu hawana ruhusa ya kuondoka makazi.

KM amepongeza Serikali ya Marekani kwa kutangaza uamuzi wa kujiunga tena na Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu. Alikumbusha KM Baraza la Haki za Bindamu ni chombo cha kimataifa muhimu katika kutunza na kulinda haki za binadamu za walimwengu wote, kote duniani, na alisisitiza Marekani inamiliki mchango muhimu utakaosaidia kuyatekeleza malengo ya Baraza hilo.

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limeripoti kupungua kwa kiwango kikubwa kabisa zile shtumu kuhusu tabia mbaya dhidi ya watumishi wa UM nchini. Kadhalika, MONUC imeripoti watumishi 31,000 wanaoambatana na shughuli za UM katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) wamefanikiwa kupataiwa mafunzo na maelekezo kuhusu makosa ya unyanyasaji na unyonyaji wa kijinsiya.

Balozi Claude Heller wa Mexico amedhaminiwa wadhifa wa Uraisi wa duru wa Baraza la Usalama kwa mwezi Aprili. Alkhamisi Balozi Heller atakuwa na mkutano na waandishi habari kwenye Makaom Makuu ya UM kuzungumzia ratiba ya kazi za Baraza la Usalama kwa mwezi wa Aprili.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter