Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UNAMID wavamiwa kwa ghafla huko Darfur

Walinda amani wa UNAMID wavamiwa kwa ghafla huko Darfur

Ujumbe wa pamoja wa walinda amani wa UM na Umoja wa Afrika, UNAMID huko Sudan Magharibi, umesema walinda amani walivamiwa kwa ghafla na watu watano au sita waliokuwa na silaha Jumatatu jioni, wakati wakisafiri kwa gari karibu na mji wa EL- Geneina huko darfur magharibi.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNAMID, Noureddine Mezni, walindaamani watatu kutoka Nigeria, na mmoja kutoka Rwanda walisafirishwa kwa helikopta hadi kambi kuu katika mji wa EL-fasher kwa ajili ya matibabu huku mwanajeshi mmoja akiwa katika hali mahututi. Msemaji wa jeshi la walinda amani alisema Darfur Magharibi imeshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ujambazi na mashambulizi mengine madogo katika wiki za hivi karibuni lakini shambulizi la jumatatu limetia wasiwasi mkubwa. "Wakati huu, walinda amani wetu walilengwa. Kabla ya hapo ilikuwa ni suala la wizi wa magari kwa kutumia nguvu au kuvunja na kuingia katika nyumba za maafisa wetu au makambi ya mashirika yasiyo ya kiserikali. Lakini wakati hili ni tukio baya sana na tunalikemea vikali, vile vile tunajaribu tuwezavyo kuwatambua washambuliaji na kuchukua hatua kali dhidi yao.

Makundi mbali mbali yenye silaha yanafanya operesheni zake katika mkoa wa Darfur hasa katika eneo la magharibi karibu na mpaka wa chad. Mbali na makundi ya waasi, na wanamgambo waoungwa mkono na serikali, yamezuka makundi ya kijambazi na kutumia nafasi ya kutokuwa na usalama katika eneo hilo kufanya operesheni zao.