Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

John Holmes, KM Mdogo juu ya Masuala ya Kiutu na Mratibu wa Misaada ya Dharura ameruhusu kutolewe dola milioni 75 kutoka Mfuko wa UM kwa Maafa ya Dharura (CERF) ili kuzisaidia nchi 14 kudhibiti hali ya dharura ilioselelea kwa muda mrefu kwenye maeneo yao. Idadi kubwa ya mchango huo, yaani dola milioni 11, zitafadhiliwa huduma za kiutu katika Zimbabwe, ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemkrasia ya Umma wa Korea (Korea Kaskazini), Ethiopia na Usomali.~

Kitengo cha UM juu ya Uchanganuzi wa Chakula kimetoa ripoti yenye kuonyesha mwaka huu watu milioni 3 ziada katika Usomali, watategemea kupatiwa misaada ya kiutu kutoka wahisani wa kimataifa ili kunusuru maisha. Ripoti ilieleza ijapokuwa hali ya wasiwasi bado imetanda nchini humo, huduma za ugawaji wa misaada ya kiutu ziliendelezwa kwa ujasiri mkubwa na washiriki wa kizalendio. Tangu mwanzo wa mwaka hadi sasa, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) lilifanikiwa kugawa, kila mwezi, tani 34,000 za chakula kwa watu milioni 3.4 katika Usomali. Shirika la Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), kwa upande wake, limejihusisha zaidi sasa hivi na ule mpango wa kuanzisha mfumo wa maji safi wa kudumu, na kuhakikisha mpango huu utasarifika. Kadhalika, UNICEF na Shirika la Afya Duniani (WHO) yanasaidia, kipamoja, kuwapatia watoto milioni 1.5, chini ya umri wa miaka 5, huduma kinga dhidi ya maradhi yanayosababishwa na maji machafu. Wakati huo huo, Ofisi ya UM inayohusika na Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba ni asilimia 18 ya misaada ya kiutu, inayohitajika kuhudumia Usomali, iliofanikiwa kufadhiliwa taidfa hilo.

Wiki ijayo Sha Zukang, Naibu KM wa UM Kuhusu Masuala ya Kiuchumi na Jamii, anatazamiwa kusafiri kwenda Namibia kufungua Mkutano wa Hadhi ya Juu Kuhusu Kilimo cha Karne ya 21 kwa Afrika. Mkutano umetayarishwa bia na Idara ya UM juu ya Masuala ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) pamoja na Serikali ya Namibia. Wajumbe watakaohudhuria kikao watasailia matatizo yaliokabili Afrika kwenye mazingira yaliofura mizozo kadha ulimwenguni, na pia watazingatia taratibu za kuyahusisha mataifa ya Afrika, kwa mafanikio, kwenye shughuli za masoko ya kimataifa ya kilimo na, hatimaye, kuimarisha maendeleo yaliosarifika katika Afrika.