Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon ameshtumu vikali mapigano yaliofumka siku ya leo baina ya kundi la waasi na Vikosi vya Ulinzi vya Sudan kwenye vitongoji vya mji wa El Fasher, Darfur Kaskazini. Uhasama huu unafuatia mpambano yaliozuka mwanzo wa mwezi baina ya Jeshi la Sudan, kundi la waasi wa JEM na jeshi la mgambo la SLA/MM. KM alitoa taarifa yenye kueleza kuchukizwa na vitendo vya uhasama vyenye kuhatarisha maisha ya raia na pia ule utaratibu wa kisiasa unaoendelezwa kwa lengo la kurudisha amani ya eneo. KM aliyataka makundi yote yanayohasimiana, kusimamisha haraka mapigano na kutekeleza kwa pamoja majukumu waliodhaminiwa chini ya sheria ya kimataifa.

Kuhusu hali katika eneo liliokaliwa la WaFalastina, katika Tarafa ya Ghaza, Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kuanzishwa, na wataalamu wa UM, shughuli za kutathminia mahitaji ya umma na ujenzi wa zile sekta za kiuchumi na jamii zilizoharibiwa na mashambulio ya karibuni kwenye eneo hilo. Hivi sasa wahudumia misaada ya kiutu katika Ghaza wamelenga kazi zai kwenye shughuli za kuwapatia wakazi waathirika wa Ghaza misaada ya kimsingi, kukidhi mahitaji ya kihali ya kila siku. OCHA imeripoti maelfu ya wakazi wa Ghaza, kwa sasa, hawana mahali pa kuishi. OCHA imearifu watu karibu 500 bado wamesalia kwenye makazi ya muda ya Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), kwa sababu wingi wa umma wa Ghaza ulion’golewa mastakimu umeamua kuishi na wenyeji wenziwao, ambao wamewasaidia mwisho wa kikomo na ilhali wao wenyewe pia wanahitajia kusaidiwa na wahisani wa kimataifa. Kwa upande wake, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeanzisha tena ile mipango ya kulisha watoto wa skuli katika Ghaza, ambapo watoto 30,000 wameanza kupewa posho ya chakula mara moja kwa siku, kwa mfululizo wa siku tano kila wiki. Posho hii inajumlisha nyama halali ya mikebe, biskuti zenye kutia nguvu na maziwa. Wakatai huo huo, msanii maarufu wa kimataifa anayeitwa Yusuf Islam, ambaye zamani akijulikana kwa jina la Cat Stevens, ametangaza Ijumatatu kufadhilia sadaka wimbo alioimba kwa niaba ya watoto wa Ghaza, wimbo ambao faida ya mauzo yake itapelekewa Shirika la UNRWA pamoja na Jumuiya ya Save the Children. UNRWA imemshukuru msanii huyo na kukaribisha kidhati mchango karimu wake ambao unatumainiwa utachangisha kwenye kazi zake za kuhudumia misaada ya kihali kwa umma muhitaji katika Tarafa ya Ghaza.

Kadhalika, Shirika la WFP limetoa msaada wa tani 650 za metriki za chakula kwa wakazi wa Kirundo, jimbo la kaskazini lkatika Burundi, umma ambao unakabiliwa na tatizo la ukame uliofuatia mvua haba zilizonyesha wakati wa baina ya Septemba na Novemba mwaka jana (2008). Msaada huu ni ziada ya tani za metriki 750 za chakula ambazo hugaiwa wanafunzi 200,000 kwenye majimbo sita mengineyo katika Burundi. Halkadhalika, Shirika la UM kuhusu Chakula na Kilimo (FAO) nail pia limetangaza litasaidia kaya kadha Burundi kupata mbegu, ikijumlisha zile mbegu za mhogo zenye kustahamili ukame, na pia kuwapatia vifaa vya kilimo.

Kwenye taadhima ya kuadhimisha Mwaka Mpya wa Kichina, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza taarifa inayohimiza raia wa Uchina kukomesha ile mila ya kupeana zawadi za sigara. WHO ilisisitiza kwamba “Kutoa zawadi ya sigireti na kufadhilia madhara.” Kwa mujibu wa takwimu za WHO wavutaji sigara milioni 350 katika Uchina hujumuisha thuluthi moja ya watu wote wanaovuta sigireti ulimwenguni.