Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahajiri wa Pembe ya Afrika waathirika tena na mbinu za wafanya magendo, yaripoti UNHCR

Wahajiri wa Pembe ya Afrika waathirika tena na mbinu za wafanya magendo, yaripoti UNHCR

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti mapema wiki hii makumi ya raia waliohajiri eneo la Pembe ya Afrika kutafuta hifadhi ya kisiasa Yemen, walizama kwenye Ghuba ya Aden kufuatia mbinu za wafanya magendo.

“Kwa uchache, tunaweza kusema, watu 20 walizama nje ya mwambao wa Yemen, hapo jana, na wawili wengine waliripotiwa kupotea baada ya wafanya magendo kuwavusha raia hawo, wa kutokea sehemu za Pembe ya Afrika, kwenye Ghuba ya Aden, ambapo waliwalazimisha kuchupa kutoka mashua waliokuwemo kwenye eneo la maji mengi.” Kwa mujibu wa Msemaji Redmond, mashua ilikuwa imechukua watu 115, wingi wao wakiwa raia wa Ethiopia .. UNHCR ilisema abiria 93 walibahatika kunusurika, na waliweza kufika nchi kavu kwenye mji wa Ahwar, uliopo kilomita 220, mashariki ya bandari ya Aden, na baada ya hapo walihamishwa kwenye kituo cha kupokea wahamiaji cha UNHCR. Wale abiria waliofariki walizikwa kwenye kiwanja kilichofadhiliwa na Serikali ya Yemen. UNHCR inasema waathirika walionusurika ajali hiyo walionekana kupigwa na kihoro kikubwa, na bumbuwazi kutokana na msukosuko huo wa safari yao, na haikuwezekana kuwahoji, kwa kina kufafanua hali halisi iliyowakabili kimaisha.